Habari za Kitaifa

Kanisa lasuta wanasiasa vigeugeu

February 20th, 2024 1 min read

NA MAUREEN ONGALA

MWENYEKITI wa Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK) tawi la Pwani, Askofu Peter Mwero, amewataka wananchi kusisitizia wanasiasa watekeleze ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Mwero alisema ni sharti wanasiasa waliochaguliwa wazingatie manifesto zao, kwani zilikuwa mojawapo ya sababu kuu za wananchi kuwachagua.

Akizungumza mjini Kilifi, alisema utekelezwaji wa baadhi ya masuala yaliyo kwenye manifesto za viongozi hao, kutaleta suluhu la kudumu kwa baadhi ya matatizo yanayokabili jamii katika sehemu mbalimbali za nchi.

“Wanasiasa walitoa ahadi kwa wananchi katika kampeni zao kuwaomba wananchi kuwapigia kura. Waliwahusisha vijana na wanawake miongoni mwa wanajamii wengine, hivyo ni wajibu wa wapigakura kuangalia manifesto ya kila mwanasiasa kama inaendelezwa kulingana na matakwa ya jamii,” akasema.

Askofu Mwero alieleza kuwa imebainika kuwa wanasiasa wengi ni vigeugeu na hawajatekeleza ahadi zao kwa vijana na wanawake jinsi walivyoahidi wakati wa kampeni.

“Tumegundua ya kwamba wakati wa kampeni, wanasiasa wanasema mambo tofauti na pindi tu wanapochaguliwa wanageuka na kuanza kutekeleza mambo tofauti,” akasema.

Wakati huo huo, kiongozi huyo aliwashinikiza viongozi wa kidini katika jamii kuwasilisha matatizo ya wananchi kwa viongozi wakuu serikalini wakati wanapofanya mikutano na wanasiasa walio kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kwenye serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

“Kama viongozi wa dini mko katika nafasi nzuri ya kujumuika na viongozi mbalimbali katika vikao tofauti ambapo imekuwa vigumu kwa vijana kuwafikia. Ikiwa utamfikia gavana, wasilisha matakwa ya vijana na wanawake,” akashauri.

Alisema hayo kwenye kongamano la viongozi wa kidini na vijana.

Linaendelea huku baraza hilo likibaini ya kwamba kaunti za Pwani bado zinakabiliwa na changamoto ya miundomisingi duni, ukosefu wa ajira, ukosefu wa huduma muhimu kwa jamii na baa la njaa licha ya ahadi za kuboresha maswala hayo kutoka kwa viongozi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

[email protected]