Habari Mseto

Kanisa lataka vikosi vya polisi vishirikiane kuzima uhalifu

July 14th, 2019 1 min read

Na SAMMY KIMATU

KANISA lina imani kuwa kikosi cha polisi kilicho na mseto wa polisi wa kawaida na polisi tawala kitabadilisha huduma kwa wananchi wakati huu waziri wa usalama Dkt Fred Matiang’i anapoleta mabadiliko katika huduma ya polisi.

Aidha, waliokuwa katika kikosi cha polisi tawala wana nafasi ya kupewa vyeo kama wakuu wa vituo vya polisi baada ya kuhamishwa.

Hayo yalinenwa Jumapili na Askofu George Kamunya wa kanisa la Oasis of Grace wakati wa ibada ya Jumapili, katikati mwa jiji, Kaunti ya Nairobi.

Askofu Kamunya aliongeza kwamba wananchi watakaposhirikishwa katika mikutano ya mseto wa maafisa hao kutawapatia mwanya wa kujihisi polisi ni marafiki na kumaliza taswira ya awali wakati polisi alipoonekana na raia kama adui.

“Mabadiliko katika kikosi cha polisi yatazaa matunda na raia atakuwa huru kutoa habari kwa polisi huku akijihisi polisi ni rafiki ya mwananchi ikilinganishwa na miaka ya hapo nyuma,” Askofu Kamunya akasema.

Kuhusu ufisadi, aliomba serikali kupiga msasa bei ya bidhaa kabla ya kuwalipa waliopewa kandarasi na serikali ili pesa za mwanasi siziporwe.