Habari Mseto

Kanisa launga mkono kuadhibiwa kwa wazazi wa watahiniwa wanaojifungua

November 6th, 2018 2 min read

Na Victor Otieno

KANISA la Kianglikana nchini limeunga mkono mpango wa serikali kuwaadhibu wazazi ambao wana wao wa kike hupachikwa mimba kisha wao hukosa kuwaripoti wanaohusika kwa polisi.

Askofu Mkuu wa kanisa hilo Jackson Ole Sapit alisema kwamba idadi ya juu ya watahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) waliojifungua wakati wa mtihani huo ni dhihirisho tosha kwa taifa kwamba hatua za haraka zinafaa kuchukuliwa kulinda wasichana dhidi ya watu walio na nia ya kuvuruga na kuharibu maisha yao.

“Hii ni ishara tosha kwamba jamii zetu hazithamini maadili tena. Hukumu kali lazima iwakabili wahusika wote ikiwemo wazazi au walezi wa watoto hao ili kuwa funzo kwa wengine wasiochukulia suala hili kwa uzito unaostahili,” akasema Bw Sapit.

Askofu huyu alikuwa akizungumza mjini Kisumu alipomtawaza Charles Ochieng’ Ong’injo kuwa askofu mpya wa Dayosisi ya Maseno Kusini aliyechukua mahala pa askofu Francis Abiero aliyestaafu.

Wiki jana katibu katika wizara ya elimu Dkt Belio Kipsang aliahidi kwamba hatua kali zitachukuliwa wazazi ambao wanao walijifungua wakati wa KCPE kwa msingi ya kutopiga ripoti kwa polisi.

“Tutaenda kwa vijiji hivyo ambavyo watu hutatua kesi hizo kupitia upatanishi. Tutamkamata mtu yeyote wakiwemo wazazi wanaoshiriki makubaliano hayo bila kuzingatia hali ya maisha ya baadaye ya wanao,” akasema Dkt Kipsang mjini Nyeri.

Zaidi ya wasichana 10 walithibitishwa walijifungua wakati wa mtihani wa KCPE uliokamilika Ijumaa wiki iliyopita.

Vile vile Bw Sapit alitaka wahusika wote kutorushiana cheche za lawama na badala yake waungane kuhakikisha suala hilo linapata utatuzi.

“Hatuwezi kulaumiana kila mara kuhusu tatizo hili. Kila mtu lazima ajitwike jukumu la kusema kiini cha shida hii na namna ya kuwalinda wasichana wetu wakiwa shuleni,” akaongeza Bw Sapit.

Kwa upande wake Bw Ong’injo aliwaonya vijana dhidi ya kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na wanaowazidi umri kwasababu mahusiano kama hayo huishia katika majanga.

“Naomba msikimbile maisha ya juu kisha mjute baadaye,” akasema askofu huyo mpya.

Bw Ong’injo alitawazwa baada ya kuwashinda wapinzani wake Zephaniah Kore na Boniface Obondi kwenye uchaguzi ulioshuhudia ushindani mkali ulioandaliwa katika kanisa la ACK St Stephen’s Cathedral mjini Kisumu Agosti 25, mwaka huu.