Kanisa linaloruhusu ndoa za watoto lamulikwa na UN

Kanisa linaloruhusu ndoa za watoto lamulikwa na UN

Na MASHIRIKA

HARARE, ZIMBABWE

UMOJA wa Mataifa (UN) umelaani utamaduni wa ndoa za watoto Zimbabwe kufuatia kifo cha msichana mwenye umri wa miaka 14, baada ya kujifungua katika madhabahu ya kanisa.

Kisa hicho kiliibua ghadhabu miongoni mwa raia na watetezi wa haki za kibinadamu. Aidha, kisa hicho kiliangazia itikadi ya kuwaoza watoto katika makanisa ya Kiapostoliki, nchini Zimbabwe, ambayo pia huwaruhusu wanaume kuoa zaidi ya mke mmoja.

Afisi ya UN nchini Zimbabwe ilisema kupitia taarifa kuwa “imefahamu kwa masikitiko makubwa na inakemea vikali” hali iliyosababisha kifo cha Memory Machaya, msichana mwenye umri wa miaka 14, kutoka kijiji cha Marange, eneo la mashariki nchini humo.

“Inasikitisha kuwa ripoti hizi za kuhuzunisha za kuwadhulumu kingono wasichana wachanga ambao hawajakomaa kiumri ikiwemo kuwaoza watoto kwa lazima, zinaendelea kujitokeza na kwa hakika hiki ni kisa kingine cha kutamausha,” ilisema taarifa ya UN iliyotolewa Jumamosi.

Mmoja miongoni mwa wasichana watatu nchini Zimbabwe huenda akaozwa kabla ya kutimu umri wa miaka 18, lilisema shirika hilo la kimataifa ambalo afisi yake Zimbabwe inaunganisha mashirika yote 25 ya UN, yanayofanya kazi nchini humo.

Serikali imekuwa kwa muda mrefu ikipuuza itikadi ya ndoa za watoto. Zimbabwe ina vitengo viwili vya sheria kuhusu ndoa, Sheria kuhusu Ndoa na Sheria kuhusu Ndoa za Kitamaduni.

Kati ya sheria hizo mbili, hakuna inayofafanua kuhusu umri unaohitajika ili kuruhusu ndoa, huku sheria kuhusu utamaduni ikiruhusu ndoa za wake wengi.

Mswada mpya kuhusu ndoa ambao kwa sasa umewasilishwa bungeni unakusudia kulainisha sheria hizo, kupiga marufuku ndoa ya mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18 ikiwemo kumkamata na kumshtaki mtu yeyote anayehusika katika ndoa ya watoto.

Polisi na tume ya kitaifa kuhusu jinsia walisema kwamba wanachunguza kilichosababisha kifo cha msichana huyo.

Vyombo vya habari vilisema kwamba msichana huyo aliaga dunia mwezi uliopita lakini kisa hicho kilijitokeza wiki iliyopita baada ya jamaa wake, waliozuiwa na walinzi wa kanisa hilo kuhudhuria mazishi yake, kusimulia kisa chao kwa idhaa ya kitaifa.

Juhudi za kuwasiliana na kanisa hilo kwa jina Johanne Marange hazikufanikiwa.

Makanisa hayo ya kiapostoliki yanayokanya waumini wao kuenda hospitalini, huwavutia mamilioni ya wafuasi kupitia ahadi zao za kuponya maradhi na kuwakomboa watu kutokana na ufukara.

You can share this post!

Kega akemea Msajili kuhusu waasi JP

TAHARIRI: Kila msafiri analo jukumu la kujilinda