Kimataifa

Kanisa msalabani: Mjadala wa mapadri kuoa waibuka tena Vatican

January 9th, 2024 2 min read

ROMA, ITALIA

NA MASHIRIKA

AFISA mkuu wa Vatican amesema kanisa linapaswa kufikiria sana kuhusu haja ya kuruhusu makasisi kuoa.

Afisa huyo, ambaye kadhalika ndiye mshauri wa kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni, Papa Francis alizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari yaliyochapishwa mnamo Jumapili.

“Pengine ni mara ya kwanza ninayasema hadharani na matamshi yangu yataonekana kuwa ya uzushi kwa baadhi ya watu,” Askofu Mkuu Charles Scicluna wa Malta, ambaye pia ni katibu msaidizi katika ofisi ya mafundisho ya Vatican, aliliambia gazeti la Times of Malta.

Papa Francis amefutilia mbali uwezekano wowote wa kubadilisha sheria ya Kanisa Katoliki inayowataka makasisi kuwa waseja. Lakini si fundisho rasmi la Kanisa na kwa hivyo linaweza kubadilishwa na Papa wa baadaye.

Scicluna, labda anayejulikana zaidi kwa uchunguzi wake wa uhalifu wa unyanyasaji wa kijinsia, alibainisha kuwa makasisi waliruhusiwa kuoa katika milenia ya kwanza ya historia ya Kanisa hilo na kwamba ndoa inaruhusiwa leo katika ibada ya Mashariki ya Kanisa Katoliki.

“Kama ningekuwa na uwezo, ningerekebisha matakwa ya kwamba makasisi wanapaswa kuwa waseja,” alisema. “Tajriba imenionyesha kuwa hili ni jambo tunalohitaji kufikiria upya.”

Scicluna, 64, alisema Kanisa “limepoteza makasisi wengi wakuu kwa sababu walichagua ndoa”.

Alisema “kuna mahali” pa useja katika Kanisa lakini pia ilibidi kuzingatia kwamba kasisi wakati mwingine huanguka katika kupenda.

Kisha anapaswa kuchagua “kati yake na ukuhani na baadhi ya makuhani hukabiliana na hilo kwa kujihusisha kwa siri katika mahusiano ya kimapenzi”.

Mjadala kuhusu iwapo makasisi wa Kikatoliki waruhusiwe kuoa umekuwepo kwa karne nyingi.

Mapadre wanaruhusiwa kuoa katika kanuni za Kanisa Katoliki na pia katika Makanisa ya Kiorthodoksi, Kiprotestanti na Kianglikana.

Wapinzani wa ukuhani wa ndoa wanasema useja au ukapera unamruhusu kasisi kujitolea kabisa kwa Kanisa.

Mnamo mwaka wa 2021, Papa alitupilia mbali pendekezo la kuruhusu baadhi ya wanaume wazee waliofunga ndoa kuwekwa wakfu katika maeneo ya mbali huko Amazoni ambako katika sehemu fulani waumini huona kasisi mara moja tu kwa mwaka.