Makala

Kanisa dogo zaidi Afrika lililo Mai Mahiu, na lina viti 12 tu kama wanafunzi wa Yesu!

Na FRIDAH OKACHI August 3rd, 2024 2 min read

KANISA la Kikatoliki eneo la Mai Mahiu, limeorodheshwa kuwa ndogo zaidi Barani Afrika kutokana na viti vya mbao vilivyotengwa ambavyo huchukua idadi ya watu 12 pekee.

Kanisa hilo lililojengwa kando ya barabara ya Mai Mahiu-Naivasha, pia linafahamika kama Travelers Chapel, kwa kuwa kivutio kwa watalii.

Bw James Kuria, 68, mwenyeji wa eneo hilo, alisema wasafiri wanaotoka au kuingia mjini Nairobi wanaotumia barabara kuu ya Mai Mahiu-Naivasha, hupitia humo.

“Ni kivutio kwa wasafiri. Wengi hutumia sehemu hii kupiga picha za kibiashara na pia kufanya sherehe za harusi,” akasema Bw Kuria.

Watalii hao wakiwapa ufahamu ukubwa wa kanisa hilo.

“Tulijua ukubwa kutokana na viti tu, hadi pale mmoja wa wajenzi kutoka Nairobi alipima na kutueleza ukubwa wa kanisa hili ni futi 15 kwa 8,” akafafanua.

Kulingana naye, kanisa hilo lilijengwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia mwaka wa 1942 na Waitaliano waliokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza.

“Kuna mwanamke mmoja wa Kiitaliano ambaye alichangia pakubwa kuchora hii barabara kuu ya Mai Mahui-Naivasha. Alipigwa risasi hadi kufa. Waitaliano hao walitaka sehemu hii kutambuliwa kwa kujenga kanisa hili,” akasema Bw Kuria.

“Vifaa ambavyo vilitumiwa vilikuwa vyenye ubora mzuri. Ndio sababu jengo hili lipo imara na litazidi kuwa vivyo hivyo,” akaongeza Bw Kuria.

Ndani ya kanisa kukiwa na viti na michoro mbalimbali. Picha| Fridah Okachi

Kuria alisema michoro ya kidini nje ya kanisa hilo iliashiria Baba katika Utatu, kando na waumini wengine, Wakatoliki wakimiminika zaidi.

“Utatu huo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Wakati mwingine utapata wale Wakatoliki wenyewe wakiingia hapa na kufanya maombi.”

Hata hivyo, Waitaliano hufanya mkutano wao mara moja kwa mwaka. Hii ni baada ya waliojenga kurejea sehemu hiyo mwaka 1985 na kuweka viti vya idadi ya watu 12 ambavyo pia huashiria wanafunzi wa Yesu.

“Kabla ya miaka ya 1985 hakukuwa na viti. Wale ambao walifika sehemu hii, walilazimika kubeba viti vyao. Lakini baada ya Waitaliano hao kurudi 1985, waliweka viti hivyo,” akakamilisha.

Kando na Wakatoliki, sehemu hiyo ambayo ni ya kuabudiwa inaruhusu waumini wengine kuitumia.