Michezo

Kante arejea kikosini baada ya kupata nafuu

November 9th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Frank Lampard anatarajia kumkaribisha kiungo mahiri N’Golo Kante, Chelsea itakapokuwa nyumbani kuvaana na Crystal Palace katika uga wa Stamford Bridge hii leo Jumamosi.

Kadhalika, huenda mpakuaji Ross Barkley akarejea kikosini baada ya kupata nafuu kutokana na jeraha la goti.

Hata hivyo, kinda Mason Mount aliyeumia majuzi wakicheza na Ajax Amsterdam ataikosa mechi hiyo pamoja na Jorginho kutokana na marufuku ya kadi za manjano.

Kwa upande mwingime, Crystal Palace wanatarajiwa kumkaribisha Andros Townsend, aliyeumia begani wakicheza na Arsenal kwenye mechi iliyomalizika kwa sare.

Hii ni mechi ya nne mfululizo kwa Crystal Palace kucheza na timu ya Ligi Kuu ya Uingere za (EPL) iliyo katika kiwango kizuri.

Kumekuwa na madai kwamba timu haiwezi kuwika katika ligi hii maarufu kwa kutegemea makinda, lakini imekuwa tofauti kwa Chelsea ambayo imefanikiwa na chipukizi wengi kikosini wakiwemo Fikayo Tomori, Mason Mount na Tammy Ibrahim.

Mbali na kunga’ra, Chelsea imevutia mashabiki kutokana na soka yao ya hali ya juu, msimu huu.

Kocha Roy Hodgson amesema kwamba kikosi chake kina matatizo machache lakini atajaribu kuzuia washambuliaji matata wa Chelsea kupenya ngome yake.

Timu hiyo ilifungwa mabao kiholelana karibu na eneo la hatari katika mechi zao dhidi ya Leicester City na baadaye Arsenal.

Itakuwa mechi ya 300 kwa kocha Hodgson kama kocha na angependa vijana wake wapate ushindi ili ajiongezee raha zaidi.

Chelsea ilianza ligi vibaya kwa kushindwa 4-0 dhidi ya Manchester United, lakini tangu wakati huo, kikosi hicho kimeibukia kuwa moto wa kuotea mbali.

Crystal Palace imeshinda mechi mbili pekee kati ya 17 dhidi ya Chelsea ugenini, lakini tangu warejee kwenye ligi kuu, vijana hao wa Hogdson wameshinda Chelsea mara mbili pekee baada ya kukutana mara 12.

Hofu

Kwa upande wa Chelsea, wana uwezo wa kushinda mechi hii ya sita kwa mara ya kwanza tangu wanyakue ubingwa wa EPL kwa mara ya mwisho Mei 2017.

Lakini kuna hofu kwamba Chelsea wameshinda mechi moja pekee kati ya tano dhidi ya timu zinazomiliki nafasi za katikati jedwalini.

Kushindwa kwao pekee katika mechi 10 za mashindano tofauti kulitokea dhidi ya Manchester United katika pambano la Carabao Cup mnamo Oktoba 30.

Vijana hao wamefunga mabao saba katika mechi tano za EPL ugani Stamford Bridge msimu huu, ikilinganishwa na mabao 18 katika mechi sita za ugenini.

Mfungaji wao bora, Tammy Abraham anamfuata Jamie Vardy wa Lecester anayejivunia mabao 10, wakati Abraham akiwa na tisa.

Crystal Palace kwa upande wao, hawajashinda katika mechi zao tatu za majuzi na wameandikisha ushindi mara nane ugenini mwaka huu.