Habari za Kitaifa

Kanu yaenda kortini ikitaka irejeshewe KICC

March 10th, 2024 2 min read

NA SAM KIPLAGAT

CHAMA cha Kanu kimeanza mchakato wa kutwaa umiliki wa Jumba la Mikutano la KICC zaidi ya miongo miwili baada ya kufurushwa kutokana na amri ya Rais.

Kwenye kesi ambayo imekuwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi tangu 2020, Kanu inasema iliondolewa kwa lazima na KICC kuchukuliwa na serikali mnamo Februari 2003 kwa njia haramu.

Chama hicho kikongwe kinasema kuwa haki zake za kikatiba zilikiukwa. Kando na KICC ambayo inakalia ardhi ya ekari 1.694, chama hicho pia kimeshutumu serikali kwa kukosa kulipa deni la Sh700 milioni kwa kampuni ya Kenya Power.

Hali hii imefanya KPLC kutwaa mali ya chama hicho jijini Nakuru. Chama hicho kilizuia bila mafanikio kuuzwa kwa mali hiyo baada ya Mahakama ya Juu kukubaliana na KPLC kwenye rufaa iliyowasilishwa ambayo korti ilisema haikuwa na mashiko.

“Ni vyema kuwa mahakama ina jukumu la kikatiba kuamua mmiliki halali wa KICC kufuatia jumba hilo kuchukuliwa na serikali ilhali ni mali ya Kanu,” akasema Afisa Mkuu wa Kitaifa wa Kanu George Wainaina kupitia stakabadhi ambazo zipo kortini.

Mpango

KICC ni kati ya mashirika 11 ya serikali ambayo yameorodheshwa kubinafsishwa japo mpango huo wa serikali haujatekelezwa baada ya chama cha ODM kupata amri ya kuuzuia kortini.

Katika kesi yake, Kanu imeshatki Wizara ya Ardhi, Waziri wa Utalii, Mwanasheria wa Serikali, KICC, Tume ya Kitaifa ya Ardhi Nchini (NLC) na Kenya Power.

Kanu inasema kuwa ndio mmiliki wa ardhi ambayo KICC inapatikana baada ya kupewa ardhi hiyo mnamo Mei 10, 1969 kupitia barua iliyoandikwa na Kamishina wa Ardhi.

Pia Kanu imesema ilipewa hatimiliki ya ardhi hiyo mnamo Mei 25, 1989, kwa muda wa miaka 99.

Katika utetezi wa serikali, Timothy Waiya Mwanga, Mkurugenzi was Mipango ya Ardhi alisema kuwa Kanu haikupewa ardhi hiyo

Bw Mwangi anasema Nairobi City Square ambayo ramani yake ilichorwa mnamo 1948 ilikuwa ardhi ya umma. Ndani ya ardhi hiyo kuna jengo la Mahakama ya Juu, Jumba la Jogoo, Jumba la Harambee na Afisi za Mwanasheria Mkuu.

Nje ya Nairobi City Square ni Holy Family Basilica, City Hall na Jumba la Vigilance.

“Hii inaonyesha kuwa ardhi hiyo ilitengwa kwa shughuli za umma na afisi ambazo zimejengwa hapo bado zinatoa huduma kwa umma,” akasema Bw Mwangi.

Katika amri iliyotolewa mnamo Februari 11, 2003, serikali ilifurusha Kanu, maajenti wake na waliokuwa wakikusanya kodi katika jumba hilo kisha kutwaa usimamizi wake.

Bw Wainaina anasema kuwa Kanu bado ina hatimiliki ya ardhi hiyo ambayo haijafutiliwa mbali na serikali ilipuuza amri ya korti katika kutwaa usimamizi wa jumba hilo.

Kanu sasa inaitaka korti itangaze chama hicho kama mmiliki wa KICC na kilipwe fidia kwa muda ambao serikali iliwapokonya ardhi hiyo.