Kanuni mpya kwa walimu wa nyanjani

Kanuni mpya kwa walimu wa nyanjani

Na FAITH NYAMAI

TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) imetoa masharti ya ajira kwa nyadhifa 1,995 za walimu walio kwenye mpango wa mafunzo ya nyanjani.

Aidha, imetangaza kuongeza muda wa mwaka mmoja zaidi kwenye kandarasi za walimu wanaoshiriki ufundishaji wa aina hiyo kwa sasa.

Mkurugenzi wa TSC anayesimamia wafanyakazi, Rita Wahome, kupitia notisi iliyotumiwa wakurugenzi wote wa kimaeneo, alisema nyadhifa zilizotangazwa ni sehemu ya walimu 6,000 wanaotarajiwa kutoa huduma zao kwa shule kuanzia Januari hadi Desemba 2022.

“Nyadhifa 4,005 zilizosalia zitajazwa na walimu wa nyanjani wanaohudumu kwa sasa waliosajiliwa 2021 na ambao hawakujumuishwa kwenye nyadhifa za ajira ya kudumu zilizotangazwa awali. Maelezo zaidi kuhusu nyadhifa hizo yamo kwenye tovuti ya TSC,” alisema.

Bi Wahome alieleza kwamba katika nyadhifa zilizotangazwa majuzi, masharti ya ajira yamebadilishwa huku yale yanayohusu walimu walemavu yakiwa kwenye sehemu tofauti.

Wakurugenzi wa kimaeneo watahitajika kuunda orodha ya bajeti ya 2021/22 kutokana na orodha itakayotolewa kwenye mfumo huo baada ya kuthibitisha stakabadhi.

TSC ilitangaza jumla ya nyadhifa 1,038 za walimu wa nyanjani kwa shule za msingi na 957 kwa shule za sekondari. Ili kuhakikisha uwazi, Bi Wahome alisema kuwa watahiniwa wote ni sharti watoke kwenye orodha iliyopo kwenye mfumo huo.

Orodha hiyo pia ni sharti itolewe kwa raia wanapoiagizia kwa njia ambayo haitahatarisha mchakato wa usajili.Ili kujisajili, watahiniwa ni sharti wawe na matokeo asilia ya mtihani, majina yao pia ni sharti yawe kwenye orodha ya wanaofuzu na ni lazima wawe na stakabadhi zote husika asilia.

Katika maeneo ambapo hakuna usalama, Bi Wahome alisema wakurugenzi wa TSC katika kaunti watahitajika kushirikiana na makamishna wa kaunti ili kutoa ulinzi wakati wa mahojiano.

“Kumekuwa na matukio ya walimu walioalikwa kufukuzwa kutoka kwenye vituo vya mahojiano na shughuli za usajili kutatizwa,” alisema.

Mkurugenzi huyo wa TSC alisema kuwa kinyume na awali, hakuna mtu atakayeruhusiwa kutia saini mkataba wa maafikiano au kupewa barua ya kumruhusu kuhudumu kama mwalimu wa nyanjani kabla ya kuthibitishwa ikiwa anafaa.

Wanaotaka kujisajili wanatakiwa kufanya hivyo kufikia Septemba 27 huku wasimamizi wa kimaeneo wakihitajika kutuma orodha ya wasajiliwa iliyotolewa kwenye mfumo, katika makao makuu ya TSC kufikia Jumatatu Oktoba 18.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Rais Suluhu hasuluhishi, anavuruga

Bodaboda kutoka Kenya wafurika Uganda kwa mafuta