Habari Mseto

Kanuni mpya za ibada zapingwa na makanisa

July 11th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MAKANISA ya kiinjilisti yamelalamika kuhusu kanuni zilizotolewa na serikali kuhusu jinsi ibada zitaendelezwa kuanzia Jumanne ijayo.

Huku taifa likiendelea kupambana na janga la corona, Serikali iliagiza ibada zisifanyike zaidi ya saa moja, kusiwe na watu zaidi ya 100 maabadini, na wagonjwa na wazee wenye zaidi ya miaka 58 wasikubaliwe kuingia.

Hii ni kutokana na ushauri wa wataalamu wa afya kwamba wazee na wagonjwa huathirika zaidi wanapoambukizwa virusi vya corona.

Hata hivyo, iliamuliwa kuwa maabadi binafsi yajiamulie kama viongozi wa dini waliozidi umri huo watakubaliwa kuendesha ibada.

Lakini sasa wahubiri na waanzilishi wa makanisa ya kiinjilisti wamejitokeza kutaka wasizuiwe kuwa na waumini wengi kanisani, na vile vile wazee waruhusiwe kwenda kanisani.

Katika Kaunti ya Nakuru, wahubiri wakiongozwa na mwenyekiti wao Alex Maina, walidai Baraza la Viongozi wa Dini kuhusu Covid-19 halikuzingatia mapendekezo ya makanisa yote.

“Tunashukuru sana serikali pamoja na baraza hilo kwa maamuzi ya kufungua makanisa na misikiti tena lakini hatukubaliani na kanuni ya kuwafungia nje watu wenye zaidi ya umri wa miaka 58 na watoto wa chini ya umri wa miaka 13,” akasema Bw Maina.

Waliongeza kuwa makanisa mengine ni makubwa na yanaweza kutoshea waumini zaidi ya 100 wakiwa wamekaa umbali wa mita moja unusu.

Msimamo huo uliungwa mkono na wenzao kutoka Kaunti ya Trans-Nzoia.

“Itakuwa vigumu sana kudhibiti roho mtakatifu wakati wa ibada kwa maana ni roho mtakatifu ndiye huongoza ibada ya Mungu. Sio kutumia nguvu za kibinadamu. Vile vile serikali imefungua milango ya ibada, iache Mungu atuongoze,” akasema Askofu Joseph Ngaruia wa Kanisa la Solid Rock Fellowship mjini Kitale.

Hayo yamejiri huku madhehebu mengine yakianza kutoa mwongozo kwa waumini wao kuhusu mbinu mpya za ibada.

Naibu Mwenyekiti wa SUPKEM, Sheikh Muhdhar Khitamy alisema kila msikiti utaunda kamati itakayohakikisha kuwa maagizo yanafuatwa.

“Kamati ya msikiti itapima mita moja na nusu baina ya wanaosali ili kupatikane nafasi inayotakikana. Waumini watabeba mfuko wa kutilia viatu na misala ya kusalia. Pia, watabeba misahafu yao,” akasema Sheikh Khitamy akiwa Mombasa.

Mazulia na mazingira ya msikiti na yatanyunyuziwa dawa mara kwa mara. Pia, milango itabakia wazi wakati wa ibada ili kuwe na hewa safi, na wanaoenda kusali watatakikana kuvaa barakoa wakati wote.

“Hakutakuwa na mkusanyiko wa watu kwenye mazingira ya msikiti baada ya ibada. Pia, ugavi wa chakula na vinywaji hautaruhisiwa kabisa ndani na nje ya misikiti,” baraza hilo likasema.

Kanisa la Africa Gospel Church (AGC) lilitangaza litanakili majina, nambari za simu na anwani za kila mtu atakayeenda kanisani.

Askofu Robert Lang’at alisema kanisa hilo limefutilia mbali mahubiri ya hadhara, harambee, makongamano, ibada za katikati ya wiki na makambi.

Kanisa la Presbyterian (PCEA) kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu, Bw Paul Kariuki ilisema waumini watahimizwa kutoa sadaka kielektroniki.

“Wale walio na pesa taslimu wataziweka kwenye visanduku vya sadaka wakati wakiondoka kanisani,” ikasema ratiba mpya ya ibada.

Mahubiri yatakuwa yakifanywa kwa dakika 20 pekee, huku dakika zilizosalia zikigawanyiwa shughuli nyingine kama vile maombi, matangazo na nyimbo za sifa ambazo kila moja zitachukua kati ya dakika mbili na dakika nane.

Ripoti za Osborne Manyengo, Diana Mutheu, Francis Mureithi, Valentine Obara na Phyllis Musasia