Makala

Kanuni za kuchinja Siku ya Idd kubwa

July 25th, 2020 3 min read

Na HAWA ALI

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swallallahu ‘Alayhi Wasallam, Maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyama. Leo ni Sikukuu ya Eid-il-Adhwha na ni muhimu kujua kanuni za kuchinja katika siku hii adhimu.

Neno Udhiyyah la Kiarabu linatokana na mzizi wa herufi tatu daad-haa-alif, ambazo huwakilishwa kama d*h.*aa yenye maana ya katikati ya Asubuhi.

Maana ya kilugha ya al-udhiyyah ni mnyama anayechinjwa siku ya Id-ul-Adhwha. Kisheria, udhiyyah maana yake ni mhanga unaofanywa kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu katika siku mahususi na kwa kutimiza masharti fulani.

Mnyama yoyote achinjwaye siku nyingine kwa ajili ya Mwenyezi Mungu si udhiyyah. Hata mnyama anayechinjwa siku ya Idd Kubwa lakini bila kuelekeza nia kwa Mwenyezi Mungu kama vile mnyama anayechinjwa kwa ajili ya kuuzwa buchani, huyo si udhiyya.

Kuchinjwa huko kwa udhiyya katika masiku ya kuchinja (ayyam al-nahr, tarehe 10, 11, 12 na 13 ya Dhul-Hijja ni jambo lililoamrishwa katika Uislamu kuwa ni sehemu ya ibada ya Hijja.

Qur’an, Sunna na Ijmaa vyote vinathibitisha jambo hilo. Kwa upande wa Qur’an, Mwenyezi Mungu, katika sura ya 108-Al-Kawthar, aya ya pili, anasema,“Basi swali kwa ajili ya Mola wako, na uchinje (kwa ajili ya Mola wako)”.

Hiyo ni amri iliyotolewa kwa Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, ambayo inasimama kama amri kwa waumini wote. Kwa upande wa Sunna ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, ilikuwa ni mila yake na mila ya Maswahaba wake na wafuasi wao waandamizi kuchinja mnyama (mara nyingi kondoo) katika Siku ya Idd Al-Adha.

Zipo riwaya nyingi mno za Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, zinazothibitisha kuwa Mtume na Maswahaba wake walichinja Siku ya Idd na kuwaamrisha wengine kufanya hivyo.

Hekima

Hekima ya Al-Udhiyyah haiwezi kufahamika kwa wanadamu kwa ukamilifu. Hata hivyo, sehemu fulani ya hekima hiyo yaweza kufahamika. Mosi, ni ishara ya shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuumba.

Pili, ni uhuishaji wa mila ya Ibrahim (as), Baba wa Manabii. Hivyo, Muumini anapochinja, anakumbushwa namna Ibrahiim (as) na Ismail (as) walivyotii kwa subira kubwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Utii wa Ibrahim kukubali kumchinja mwanawe kipenzi, na utii wa Ismail kukubali kuchinjwa ni masomo kwa Waumini kwamba wawe tayari kuvitoa vipenzi vyao na kuyatoa muhanga maisha yao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Tatu, Al-Udhiyyah ni tendo linalopingana waziwazi na wale wanaosema kuwa ni haramu kwa wanadamu kuchinja wanyama na kula nyama kwani kitendo cha kuwachinja kinawaumiza wanyama na kinahujumu utukufu wa maisha yao.Nne, Al-Udhiyya inabainisha kuwa njia ya huruma zaidi ya kumuua mnyama ni kumchinja.

Na tano, Al-Udhiyya inazidisha shukurani ya Muumini kwa Mwenyezi Mungu kikiwa ni kiashiria cha namna Mwenyezi Mungu alivyoutiisha ulimwengu kwa wanadamu na kuuhalalisha uhai wa wanyama kwao ili wapate manufaa mbalimbali.

Kwa undani wake, udhiyyah ni ibada iliyokokotezwa katika Sunna ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam. Ni Sunna Mu’akkadah, hivyo ndivyo idadi kubwa ya Maulamaa wanavyosema.

Masharti yake ni pamoja na mtu anayechinja lazima awe Muislamu, awe mkaazi, na asiwe msafiri, awe mtu mwenye uwezo kifedha, awe mtu mzima na mwenye akili timamu.

Masharti ya kusihi

Masharti ya kuswihi kwa Udhiyyah ni pamoja na mnyama anayechinjwa awe yule anayefugwa; ng’ombe, kondoo, mbuzi, nyati maji na kadhalika, mnyama anayechinjwa lazima awe ametimiza miezi 6 ikiwa ni mbuzi, mwaka mmoja ikiwa ni kondoo, miaka 3 ikiwa ni ng’ombe, na miaka 5 ikiwa ni ngamia, mnyama asiwe na hitilafu hasa zile zinazoweza kuathiri nyama yake.

Muda wa kuchinja huanzia Alfajir, hata hivyo, uchinjaji uanze baada ya Swala ya Idd. Sunna ya kuchinja ni kuiacha damu ya mnyama imwagike.

Ugawaji wa nyama ni kwamba; theluthi moja ni sadaka ya masikini, theluthi moja ni zawadi kwa majirani, ndugu na jamaa, na theluthi moja kwa ajili ya nyumbani kwa mtu mwenyewe.

Mgawanyo uwe sawasawa lakini kama mahitaji ya nyumbani ya mchinjaji mwenyewe ni makubwa, basi mchinjaji achukue sehemu kubwa.

Au kama ana ndugu fukara wa nasaba, basi sehemu kubwa awape ndugu. Kama yeye mwenyewe si muhitaji wa nyama hiyo, basi sehemu kubwa atoe Swadaka.