Makala

‘Kanuni za ushemeji’ anazofaa kuzingatia mwanamke anapoolewa

March 20th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

JE, ni kanuni zipi ambazo mwanamke aliyeolewa anafaa kuzingatia ili kuhakikisha ana uhusiano mzuri na mashemeji wake?

Mbona baadhi ya wanawake hukosana na mashemeji wao wanapoolewa?

Hayo ni miongoni mwa mafumbo ambayo yameibukia kuwa magumu kwa wanawake wanaoingia kwenye ndoa bila mwongozo maalum.

Hata hivyo, kulingana na Pasta Sue Munene, ambaye ni mshauri wa masuala ya ndoa na mahusiano, kuna kanuni kadhaa ambazo mwanamke anafaa kuzingatia ili kuboresha uhusiano baina yake na mashemeji wake.

Je, kanuni hizo ni zipi?

Kwanza, lazima mwanamke afahamu kuwa kwa asilimia kubwa, hawezi kuwabadilisha mashemeji wake.

Kulingana na Pasta Munene, lazima mwanamke afahamu kuwa anapoolewa, kuna mtindo wa kimaisha na desturi maalum ambazo mashemeji hao walikuwa wakizingatia kabla yake kuolewa.

“Lazima afahamu njia ya kukubali kuheshimu mtindo wao wa kimaisha,” akasema Bi Munene.

Pili, lazima mwanamke aishi na mashemeji wake kwa uungwana. Hapa, mwanamke anafaa kufahamu kuhusu ikiwa mashemeji wake wana sifa ya kukasirika haraka au ni watu wachangamfu. Kwa hili, itakuwa rahisi kwake kuingiliana nao bila tatizo lolote.

Tatu, lazima mwanamke afahamu na kuweka mipaka kwenye mahusiano baina yake na mashemeji wake.

Pasta Sue Munene. PICHA | WANDERI KAMAU

“Ni vizuri mwanamke afahamu kuwa yuko kwenye ndoa, na mtu pekee anayefaa kuingiliana naye bila mipaka, ni mumewe wala si ndugu zake. Kwa hili, ataeopuka mizozo ambayo huibuka mara kwa mara,” akasema.

Nne, mwanamke anafaa kuepuka kujibizana na mama mkwe, baba mkwe au ndugu za mumewe.

“Ikiwa kwa namna moja watu hao wamemkasirisha, anafaa kumwambia mumewe ili azungumze nao, badala yake kuwazungumzia moja kwa moja. Hilo litadumisha hekima baina yake na wakwewe,” anaeleza.

Tano, mwanamke hafai kujadili sifa za mumewe na mama mkwe, baba mkwe au shemeji yoyote yule.

Pasta Sue Munene. PICHA | WANDERI KAMAU

Pasta Munene anasema kuwa lazima mwamamke afahamu kuwa yeye ni ‘mgeni’, ila mume wake na ndugu zake wana uhusiano wa damu.

“Haitakuwa vigumu kwa ndugu hao kumwambia mumewe waliyozungumza kumhusu,” asema.

Sita, ni vizuri mwanamke kujifunza kumnunulia mama au baba mkwe zawadi mara kwa mara. Kwa hili, ataongeza mshikamano na kutia nguvu mahusiano yaliyomo baina yake na mashemeji wake.

Saba, si vizuri mwanamke kukaa kwa muda mrefu na mama mkwe au dada za mume wake.

“Hata ikiwa watu hao watamtembelea, hawafai kukaa kwa muda mrefu katika nyumba yao. Hili litahakikisha kuwa wanaheshimiana,” anaeleza.

Nane, ni vizuri mwanamke kujua namna ya kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza. Kulingana na Pasta Munene, mbinu hii huwa inampa nafasi mwanamke kuwajua zaidi mashemeji wake ili kuepuka hali zozote ambapo wanaweza kukwaruzana.

Mwisho, ni vizuri mwanamke ajenge mtindo wa kumrai mumewe kuwatembelea wazazi wake kila mara anapopata muda.

“Ni vizuri mwanamke awe akiandamana na mumewe, kwani hilo hujenga uhusiano mwema baina yake na wakwe zake,” anashauri.