Makala

KAPEDO: Uhalifu wasababisha upungufu wa chakula

May 15th, 2018 2 min read

Na SAMMY LUTTA

WAKAZI wa maeneo ya Kapedo na Lomelo katika Kaunti ya Turkana wamelazimika kutegemea chakula cha msaada kutokana na uvamizi wa mara kwa mara katika barabara za mpaka wa kaunti hiyo na Baringo.

Wavamizi hujificha kando ya sehemu za barabara kuu na kushambulia magari kutoka Marigat, Kaunti ya Baringo na Lokori iliyo Turkana.

Shambulio la majuzi zaidi lilitokea katika eneo la Ameyan katika barabara ya Marigat kuelekea Kapedo ambapo wanafunzi watatu na dereva waliuawa kwa risasi hapo Mei 4.

Wanafunzi hao walikuwa wakirudi shuleni Kapedo.

Bw Joshua Loyanae alisema wanakumbwa na njaa kwa sababu ya uhaba wa chakula kwani kwa miezi mitatu iliyopita hali duni ya usalama imefanya maduka yafungwe baada ya bidhaa za kuuza kuisha.

“Hatuna mahali popote pa kununua chakula hata kama tuna pesa. Biashara na usafiri zimeathirika vibaya na wizi wa barabarani na hakuna yeyote anayetaka kuhatarisha maisha yake,” akasema.

Kamishna wa Kaunti ya Turkana, Bw Seif Matata, jana alithibitisha kuwa wizi wa barabarani umeongezeka katika barabara hiyo.

Kulingana naye, imebidi maafisa wa usalama wabadilishe mbinu zao za kupiga doria ili kukabiliana na wahalifu hao na akahakikishia wananchi kwamba watapewa ulinzi wa kutosha wanapotaka kusafiri.

“Kwa wafanyabiashara wanaotegemea masoko ya Marigat na Baringo, maafisa wa usalama wa Kaunti za Baringo na Turkana watashirikiana kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanapewa ulinzi wanaposafiri kuelekea au kutoka Kapedo,” akasema.

Alisema serikali inategemea wanajeshi wa KDF kusafirisha chakula cha msaada na bidhaa zingine muhimu kwa wakazi wa Lomelo na Kapedo.

Kamishna alionya viongozi wa jamii za Turkana na Pokot wakome uchochezi kwenye mitandao ya kijamii na wakubali kuheshimiana na kuungana kueneza amani.

Diwani wa wadi ya Kapedo/Napeitom, Bw Willy Nalimo, alisema wakazi hao wamekuwa wakikumbwa na njaa kwa sababu bidhaa ziliisha madukani katika masoko hayo mawili.

“Ni sharti serikali itambue kuna dharura na wakazi wa Kapedo na Lomelo wanahitaji kutendewa haki yao ya kupewa usalama sawa na Wakenya wengine nchini kote. Mtu yeyote anayechochea na kufadhili wizi wa barabarani pia anafaa kukamatwa,” akasema Bw Nalimo.