Habari za Kitaifa

Kapteni Litali alifariki akisubiri kupandishwa cheo kuwa meja

April 19th, 2024 1 min read

Na JOSEPH OPENDA

FAMILIA ya Kapteni Hillary Shirekule Litali, aliyeangamia katika ajali ya ndege Alhamisi, imemtaja kama mchangamfu, mwenye nidhamu na kujituma, mcha Mungu na aliyeiweka familia yake mbele.

Kapteni Litali, 29, ambaye ni kifungua mimba wa Bw Dickson na Bi Evelyn Litali kutoka eneo la Shabab, Kaunti ya Nakuru, alikumbana na mauti pamoja na Mkuu wa Majeshi, Francis Ogola, katika ajali iliyofanyika kwenye mpaka kati ya Kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi.

Wazazi wa Kapteni Hillary Litali, Dickson Litali na Everline wakiwa na majonzi mengi nyumbani mtaa wa Shabab, Nakuru wakionyesha picha ya mwanajeshi huyo aliyeangamia kwenye ajali ya helikopta. Picha|Boniface Mwangi

Kabla ya kifo chake, Kapteni Litali aliyejiunga na jeshi mnamo 2013, alikuwa anasubiri kupandishwa cheo kama Meja.

Alihudumu kama msaidizi chini ya majenerali wawili wa jeshi, Jenerali Robert Kibochi na Jenerali Ogolla.

“Nilikuwa na matarajio makuu kwake. Tulikuwa na uhusiano wa karibu mno, tuliwasiliana kila siku na alikuwa na ari ya kubadilisha maisha ya familia,” alisema Bw Litali kuhusu mmoja wa wanawe wawili.

Bw Litali aliwasiliana na mwanawe Jumatatu ambapo alimfahamisha kuhusu kazi ya Elgeyo Marakwet pasipo kujua yangekuwa mazungumzo yao ya mwisho.