Habari za Kaunti

Karani alitoa Sh1.8 milioni za mishahara kinyume cha sheria kaunti ya Kisii


ALIYEKUWA Karani wa Bunge la Kaunti ya Kisii James Nyaoga aliamuru kutolewa kwa Sh1.8 milioni zilizotengewa malipo ya mishahara ya wafanyakazi kwa matumizi mengine yasiyokusudiwa kinyume cha sheria, madiwani wa kaunti hiyo wamebaini.

Kosa hilo lilifanyika kati ya Juni 1, 2022 na Juni 20, 2022.

Pesa hizo zilikuwa zimehamishwa hadi kwa akaunti ya kibinafsi, kinyume na Kifungu cha 154 (1) (c) cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ya 2012.

Maelezo hayo yako katika stakabadhi zilizowasilishwa katika Bunge la Kaunti ya Kisii mnamo Alhamisi wiki jana.

Baadaye madiwani walipitisha hoja ya kumtimua afisini Bw Nyaoga.

“Pesa zilizohamishwa hadi akaunti yake ya kibinafsi zilinuiwa kuwekwa katika Chama cha Akiba na Mikopo cha Wafanyakazi wa Bunge la Kaunti. Kwa hivyo hatua hiyo ni uhalifu wa kiuchumi kwa mujibu wa sheria ya kupambana na ufisadi,” akasema Diwani wa Wadi ya Bassi Bogetauri.

Kauli hiyo pia ilishikiliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Muda iliyoundwa kuendesha uchunguzi dhidi ya Bw Nyaoga, Bw Ibrahim Machuki.

Kulingana na hoja hiyo ya kumwondoa afisini karani huyo, Bw Nyaoga aliendesha shughuli za utoaji fedha za umma katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 bila kupata idhini kutoka kwa Bodi ya Utumishi wa Umma katika Bunge la Kaunti ya Kisii.

Aidha, hakuwasilisha hilo katika ripoti ya matumizi ya fedha za umma kinyume cha hitaji la Kifungu cha 149 cha Sheria ya Usimamizi wa Pesa za Umma ya 2012.

Kwa hivyo, madiwani walioamua kwamba Bw Nyaoga alikiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba (kuhusu maadili) na Sheria ya Utumishi wa Umma katika Bunge la Kaunti ya 2017.

Karani huyo pia alitimuliwa kwa kosa la kudhihirisha mienendo mibaya kazini.

Bunge hilo pia lilisema kuwa Bw Nyaoga alikataa kuchunguzwa na Bodi ya Utumishi baada ya wafanyakazi 100 kumshutumu kwa matumizi mabaya ya fedha.

“Karani alipoalikwa na Bodi kutoa maelezo kuhusu suala hili, aliikaidi. Kwa hivyo, bunge hili limeamua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 20 (3) na kifungu cha 43(1) (f) cha Sheria ya Utumishi wa Bunge,” hoja hiyo ikasema.