Habari Mseto

Karani wa korti auawa kwa njia ya kusikitisha

May 6th, 2019 1 min read

Na TITUS OMINDE

POLISI mjini Eldoret mnamo Ijumaa walipata mwili wa karani wa mahakama kuu ukiwa umetupwa kilomita chache kutoka katika nyumba yake mtaani Action, kando ya barabara kuu ya Eldoret -Iten.

Marehemu David Ouma, 26, alikuwa karani wa Jaji Hellen Omondi.

Mke wa marehemu ambaye alikuwa amelemewa na majonzi alisema mume wake alitoka nyumbani usiku mwendo wa saa tatu usiku alipopokea simu kutoka kwa mtu ambaye alimtambua kama rafiki yake.

Bi Ouma alisema baada ya mume wake kukaa nje kwa muda mrefu alijaribu kumpigia simu bila kufanikiwa.

Hatimaye aliitwa katika hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH) ambapo alishtuka kupata mwili wa mume wake ukiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini humo.

“Nilishtuka kupata mwili wa mume wangu ukiwa mochari baada ya kutoka nje akiniambia alikuwa amepigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa nje ili wazungumze,”” alisema mke huyo kwa simanzi kuu.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya MTRH na maafisa wa polisi ambao waliuokota kutoka katika eneo la mkasa. Afisa mkuu katika eneo la Moiben, Bw Jamlek Ngaruya alithibitisha kupatikana kwa mwili huo Ijumaa usiku.

Bw Ngarunya alisema mwili huo ulikuwa na majeraha yanayoshukiwa kuwa ya kisu.

“Maafisa wetu ambao walikuwa kwenye doria usiku katika barabara ya Eldoret –Iten karibu na eneo la Block 10, hatua chache kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Eldoret, walipata mwili wa mwanaume wa umri wa makamo ukitokwa na damu. Mwili huo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi MTRH mjini Eldoret,” alisema Bw Ngurunya.