Habari

Karani wa sensa aliyechafua makazi ya mtu atozwa faini

August 31st, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

KARANI wa sensa aliyekamatwa baada ya kwenda kuwahesabu watu katika nyumba moja akiwa mlevi katika Kaunti ya Murang’a amekubali kukiuka kanuni za kazi yake.

Samson Ndirangu alikubali mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Violet Ochanda, aliyemwachilia kwa dhamana ya Sh20,000 ama kifungo cha miezi minne gerezani.

“Nimemwachilia karani huyo kwa faini ya Sh20,000 ama kifungo cha miezi minne,” akasema kwenye uamuzi wake.

Karani huyo alifika katika makazi hayo katika eneo la Mukuyu Alhamisi usiku akiwa mlevi. Baadaye, alianza kukojoa ndani ya nyumba hiyo, bila kujali uwepo wa watoto.

Vilevile anadaiwa kula chakula cha watoto hao.

Karani hakuwa na vifaa vya kuwahesabu watu wakati huo.

Katika Kaunti ya Nyeri, viongozi wa kisiasa na kidini wamewataka watu kuhakikisha kuwa wamehesabiwa kabla ya shughuli ya sensa kukamilika leo Jumamosi.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nyeri, Bi Rahab Mukami, aliwasihi wakazi wa kaunti hiyo ambao hawajahesabiwa kuwatafuta makarani na kuhakikisha kwamba wamehesabiwa kabla ya zoezi kukamilika.

“Ikiwa haujahesabiwa au makarani hawajafika nyumbani kwako, tafadhali, watafute na uhakikishe wamekuhesabu. Haupaswi kukaa tu na kusema kwamba hawakuja,” akasema Bi Mukami.

Aliwakumbusha kuwa rasilimali za nchi hugawanywa kulingana na idadi ya watu akisema kuwa kaunti zingine zinaweza kuunganishwa kwa sababu ya kuwa idadi ndogo ya watu.

Asilimia 90

Katika kaunti ya Nyandarua asilimia 90 ya wakazi walikuwa wamehesabiwa kufikia Ijumaa.

Katibu wa wizara ya uchukuzi Prof Paul Maringa na mwenzake wa mafuta Bw Andrew Kamau walisema walitarajia wakazi wote watahesabiwa kabla ya zoezi kukamilika.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Gibert Kitiyo alisema asilimia 80 ya wakazi walikuwa wamehesabiwa kufikia Ijumaa licha ya visa vya ukosefu wa usalama vilivyohudiwa eneo hilo.

Katika Kaunti ya Lamu, serikali ya kitaifa imetuma makarani zaidi wa kuhesabu watu eneo la Lamu ili kusaidia kuharakisha zoezi la sensa masaa machache kabla ya shughuli hiyo kukamilika.

Shughuli hiyo ya kuhesabu watu ilianza rasmi kote nchini mnamo Agosti 24 na imepangwa kukamilika Jumamosi Agosti 31.

Akizungumza Ijumaa na wanahabari mjini Lamu, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, alithibitisha kuongezwa kwa makarani 15 zaidi ambao tayari wamesambazwa kwenye baadhi ya maeneo ambayo yameshuhudia kujikokota kwa zoezi hilo la kuhesabu watu.

 

Ripoti za NDUNG’U GACHANE, MERCY MWENDE, WAIKWA MAINA na KALUME KAZUNGU