Michezo

Karantini ilirefusha likizo ya kocha Steven Polack – usimamizi Gor Mahia

September 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MWENYEKITI wa Gor Mahia, Ambrose Rachier amefutilia mbali tetesi kwamba wamekatiza uhusiano wa kocha Steven Polack.

Kocha huyo raia wa Uingereza aliondoka humu nchini mnamo Septemba 11, 2020, na kurejea kwao kwa likizo fupi.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya mashabiki wa Gor Mahia walifasiri kuondoka kuwa ndio mwisho wa kuhusiana na K’Ogalo – madai ambayo sasa Rachier amekana.

“Polack atarudi hivi karibuni. Aliomba likizo na sasa yuko Finland. Hata hivyo, likizo yake ilirefuka kwa sababu alilazimika kuingia karantini kwa wiki mbili,” akasema Rachier kwa kusisitiza kwamba Polack hajamfichulia lolote kuhusu mpango wa kuagana na Gor.

“Ana tiketi ya kuenda na kurudi na yuko tayari kuendelea na majukumu yake kambini mwa Gor Mahia,” akasema Rachier kwa kufichua kwamba mpango wa kujifua ambao kwa sasa unazingatiwa na wanasoka wa Gor mazoezini, ulibuniwa na Polack.

Polack alijiunga na Gor Mahia mnamo 2009 kujaza nafasi ya Hassan Oktay kwa sababu za kibinafsi.

Rachier pia ameshikilia kwamba ana imani kubwa kwa wanasoka wapya waliojiunga na Gor Mahia muhula huu na kwamba wataongoza kikosi kihifadhi taji la Ligi Kuu ya Kenya na kupiga hatua kubwa zaidi katika soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu ujao.

Licha ya kutolegezwa kwa kanuni za afya zinazodhibiti msambao wa corona, Gor Mahia wamerejelea mazoezi kwa minajili ya kampeni za muhula ujao.

“Tuliagana na idadi kubwa ya wanasoka msimu huu, lakini tulijizatiti na kujisuka upya kwa kusajili wachezaji 14 ambao naamini watajaza vilivyo mapengo yaliyoachwa.”

“Ingawa siwezi kusema kwamba tuna kikosi thabiti kuliko msimu uliopita, nahisi kwamba tumejishughulisha ipasavyo na vinara wa benchi ya kiufundi watafurahia kufanya kazi na sajili wapya.”

Baadhi ya wanasoka wapya ambao wamesajiliwa na Gor Mahia msimu huu ni Jules Ulimwengu wa Burundi, Andrew Malisero wa Malawi, Tito Okello wa Uganda, Bertrand Konfor wa Cameroon, Andrew Juma, Levis Opiyo (Nairobi City Stars), John Macharia, John Ochieng (Chemelil Sugar), Kennedy Owino, Benson Omala na Kelvin Wesonga (Western Stima).

Beki Joash Onyango aliyehamia Simba SC, kipa David Mapigano aliyejiunga Azam FC, Boniface Omondi na Peter Odhiambo waliotokea Wazito na Dickson Ambundo who returned to his native Tanzania.