Bambika

Karen Nyamu ajitetea baada ya Samidoh kufuata mkewe na watoto Amerika

January 23rd, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

SIKU ya Ijumaa, Seneta Karen Nyamu alijipata pabaya baada ya shabiki mmoja mtandaoni kushinikiza kujua alipo mpenziwe Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Seneta huyo alilazimika kufichua kwenye chapisho lake la Facebook na kutangaza kuhusu ziara ya Samidoh kusafiri Amerika kuwaona watoto wake.

Kwenye chapisho hilo, alitumia fursa hiyo kubainisha wazi hatakuwa na tatizo lolote iwapo mwimbaji huyo wa mtindo wa Mugithi ataamua kusuluhisha mambo na mke wake wa kwanza, Bi Edday Nderitu.

“Tunapozungumza yeye yuko pale kuwaona watoto wake. Edday, pia akirudi kwa mix, tumeshare miaka mingi sana kwa amani hakutakuwa na tatizo,”  alisema Karen Nyamu.

Mwanasiasa huyo alieleza mashabiki wake kuwa hangeweza kujiunga na Samidoh akiwa na familia yake nyingine nchini Amerika kwa kuwa angeharibu mambo, kinyume na matakwa yao.

Jumatatu asubuhi, ilibainika wazi baba huyo wa watoto watano yupo mjini Boston, kukutana na watoto wake baada ya muda mrefu.

Hii ni baada ya bintiye Shirleen Muchoki kufichua habari za mkutano wao kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuelezea furaha yao kwa kukutana naye.

Wow, siku njema sana, babangu hatimaye yuko hapa, tumekukosa sana baba, karibu Boston,” alipakia Shirleen.

Hii ni mara ya kwanza kwa Samidoh kukutana na watoto wake baada ya familia yake kuondoka nchini Kenya Mei 2023.