Makala

Karibu Kobala, kijiji ambako watu huishi na wafu

Na ZEYNAB WANDATI August 19th, 2024 2 min read

WAKAZI wa kijiji cha Kobala katika Kaunti ya Homa Bay wanaishi na mifupa ya wafu iliyofukuliwa na wachimbaji changarawe ambao wamesababisha matimbo makubwa na kuacha nyumba zikining’inia na makaburi yakiwa wazi.

Ni jambo la kawaida kupata sehemu za majeneza, mifupa ya binadamu au vipande vya nguo vikitoka ardhini unapotembelea kijiji hicho. Hapa, wafu hupumzika vipande vipande.

‘Hali ya Kobala ni mbaya sana,’ mkazi Willis Omullo anasema. ‘Haya yote yalianza miaka 15 iliyopita wakati uchimbaji wa mchanga ulipokithiri. Leo, angalau robo ya kijiji imechimbwa. Hata makaburi hayajasazwa.’

Omullo alikulia Kobala na amejionea mwenyewe jinsi mazingira yalivyobadilika huku uhitaji wa mchanga ukimomonyoa mfumo wa ikolojia.

Katika baadhi ya maeneo, uzoaji wa mchanga unafanyika chini ya kiwango cha maji ya ziwa, na sasa maeneo makubwa ya ardhi yametelekezwa huku ziwa hilo likichukua kulikochimbwa.

‘Miaka 15 iliyopita kulikuwa na nyumba nane katika eneo hili,’ anasema akiashiria eneo kubwa la kinamasi. Limemea makunjo juu ya udongo wenye msalaba mweupe.

‘Ndio, hilo ni kaburi,’ anasema, akionyesha msalaba mweupe. ‘Kaburi hilo lilikuwa karibu na nyumba lakini kufuatia miaka mingi ya uchimbaji mchanga na uharibifu, nyumba hiyo iliharibiwa na kaburi likaachwa likining’inia,’ anasimama kwa muda, akitazama kaburi hilo.

‘Familia zilizoishi hapa ziliondoka miaka mingi iliyopita na huenda zisirudi nyumbani.’

Inasikitisha kuona ukubwa wa uharibifu unaokikumba kijiji. Willis ananiongoza hadi kwenye uwanja uliofurika kiasi. Karibu na ua kuna kizuizi cha simiti, ambacho ananiambia kilikuwa sehemu ya jiwe la msingi.

‘Ukiangalia jiwe la simiti, unaona jina la mtu aliyezikwa hapa. Alikuwa mchungaji, alizikwa Januari 1986. Kaburi hili hapa lilifukuliwa kabisa, halijaning’inia,’ anasema.

‘Unamaanisha nini, limefukuliwa kabisa?’ Namuuliza. ‘Je, familia yake ilikuja kuchukua mabaki yake au wachimbaji mchanga walimfukua?’

‘Hapana,’ anasema kwa uthabiti. ‘Ni familia zenyewe ndizo zinachimba sio wageni, hii yote ni ardhi ya familia, kwa hiyo kila ukiona nyumba inaning’inia au kaburi limeharibiwa, ni familia yenyewe inafanya hivyo, imekuwa mbaya sana, tumepoteza heshima kwa wafu,’ anasema.

Futi chache kutoka kwenye jiwe la simiti tunalotazama ni sehemu nyingine ya simiti.

‘Je! vipande hivi viwili vilikuwa vimeunganishwa?’ namuuliza Willis.

“Ndio. Sasa hatujui kama mabaki ya huyu jamaa kama bado yapo. Kama yapo, hayupo sehemu moja. Kuna uwezekano mkubwa wa kuwa vipande vipande. Familia nyingi hapa haziwezi kupata makaburi ya wapendwa wao kwa sababu ya uzoaji wa mchanga.’

Tunapotoka kwenye kaburi la mchungaji, bibi kikongwe anatusogelea. Yuko njiani kuelekea sokoni lakini anataka kujua kwa nini tuna kamera. Anazungumza Kiluo pekee na hivyo Willis anamweleza tunachofanya, na kumuuliza kama angependa kutueleza hadithi yake. Anaitikia kwa kichwa.

‘Jina langu ni Karen Juma Odera kutoka lokesheni ndogo ya Kobala,’ anasema. ‘Nilikuwa mchimbaji wa mchanga, na hapa ndipo nilipopata pesa za kusomesha watoto wangu na hata chakula.

Kwa bahati mbaya, nilikuwa na sehemu ndogo ya ardhi, kwa hiyo niliimaliza na kuacha kuchimba mchanga. Nilipokuwa kwenye biashara ya kuuza mchanga, ilinichukua siku nne kujaza lori, na baada ya hapo ningelipwa Sh1,000.

Kazi yangu kubwa wakati huo ilikuwa kusafirisha mchanga hadi kwenye lori. Hivi ndivyo nilivyonusurika. Haikutosha, lakini angalau nilipata kitu mwisho wa siku,’ anasema.