Michezo

Kariobangi Sharks waanza vizuri safari ya kutetea taji la SportPesa Shield

March 16th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KARIOBANGI Sharks wameanza kutetea taji la soka ya SportPesa Shield kwa kishindo Jumamosi baada ya kupapura wenyeji wao Elim kwa mabao 5-0 uwanjani Bukhungu mjini Kakamega.

Mabao mawili kutoka kwa Henry Juma na moja kutoka kwa mchezaji mpya Nicholas Omondi, mwanasoka bora wa Kenya mwaka 2018 Eric Kapaito na Sydney Lokale yalitosha kuipa Sharks ushindi huo muhimu katika raundi ya 32-bora.

Mshindi wa kombe hili hutunukiwa Sh2 milioni na wadhamini, kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa, na pia tiketi ya kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho la Afrika.

Sharks ilifika raundi ya kwanza ya mashindano haya ya daraja ya pili ya Afrika baada ya kubanduliwa nje na Asante Kotoko ya Ghana.

Ilikuwa imeondoa Arta Solar7 ya Djibouti katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza.

Vijana hawa wa kocha William Muluya walikuwa wanashiriki mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yao.