Michezo

Karius aelekea Union Berlin kwa mkopo

September 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIPA wa Liverpool, Loris Karius amekamilisha uhamisho wake hadi Union Berlin ya Ujerumani kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 27 alitamatisha ghafla mkataba wake wa mkopo kambini mwa Besiktas ya Uturuki mnamo Mei 2020. Wakati huo, kandarasi yake ya miaka miwili kambini mwa Besiktas ilikuwa karibu kukamilika.

Karius alijiunga na Liverpool mnamo 2016 baada ya kushawishiwa kuagana rasmi na Mainz kwa kima cha Sh658 milioni. Mchuano wake wa mwisho kudakia Liverpool ni fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha miamba hao wa Uingereza na wapambe wa soka ya Uhispania, Real Madrid.

Masihara ya Karius katika fainali hiyo iliyochezewa jijini Kiev, Ukraine, yalishuhudia Liverpool wakipokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa vijana wa kocha Zinedine Zidane.

Union Berlin walikamilisha kampeni za Bundesliga msimu uliopita katika nafasi ya 11 jedwalini.

Kipa mwingine wa Liverpool, Kamil Grabara, 21, ameyoyomea Denmark kuvalia jezi za AGF Aarhus kwa mkopo wa msimu mmoja.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO