Habari Mseto

Karoney akiri serikali ilitoa hati miliki zenye kasoro

May 9th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

WAZIRI wa Ardhi Farida Karoney amekiri kuwa wizara yake ilitoa hati miliki za mashamba zenye makosa katika maeneo kadhaa nchini, hali ambayo imekuwa ikiwasumbua Wakenya wengi.

Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Ardhi bungeni Alhamisi, Bi Karoney alisema kuwa baada ya malalamishi kutoka kwa Wakenya katika maeneobunge tofauti, wizara yake ilituma wataalam kupima mashamba fulani yaliyokuwa na utata na ikabaini kuwa kulikuwa na makosa katika rekodi za wizara, huku kauli za wamiliki mashamba zikiwa ndizo sahihi.

Utata mkubwa ulikuwa kuwa katika rekodi za wizara, baadhi ya mashamba yalinakiliwa kuwa madogo kuliko kiwango halisi na mengine kunakiliwa majina mabaya ya wamiliki.

Mbunge wa Mwingi ya Kati Gideon Mulyungi aliuliza swali bungeni, kuhusu ikiwa waziri huyo alikuwa anajua kuwa katika maeneo ya Mui, Enziu na Endui katika eneobunge lake hati za umiliki wa ardhi zilikuwa zikitolewa na makosa.

Bw Mulyungi alisema kuwa wakati hati za umiliki wa baadhi ya mashamba zilipotolewa, rekodi zilionyesha kuwa ni madogo kuliko ukubwa wake halisi.

Baadhi ya yale aliyotaja ni moja ambalo licha ya kuwa na ukubwa wa ekari8.5, hati ya umiliki kutoka kwa wizara ilionyesha kuwa ni la ekari 2.18 na jingine la ukubwa wa ekari 4.9, lakini hati ikasema ni la ukubwa wa ekari 2.2.

Waziri Karoney alikiri kuwa wakati wizara ilituma maafisa wake kupima mashamba hayo, ilipata kuwa ni kweli yalikuwa jinsi wamiliki wanadai

“Wakati wa kunakili habari za vipande vya ardhi katika maeneo hayo, makosa yalifanyika katika mashamba kadhaa. Wamiliki wa mashamba hao halisi wameombwa kujulisha msajili wa ardhi katika kaunti ili marekebisho yafanywe,” akasema Bi Karoney.

Waziri huyo aidha alisema kuwa ameamrisha mkurugenzi wa usoroveya kuhakikisha kuwa mashamba hayo yote yanapimwa tena, ili makosa yajulikane yalipo.

Wabunge wa kamati hiyo walisema kuwa masuala kama hayo yanawaathiri Wakenya wengi, wakimshauri Bi Karoney kuwa akiandaa kliniki za mashinani, kwa lengo la kuwaalika watu walio na matatizo ya umiliki wa mashamba kuhudumiwa huko.

“Kumekuwa na matatizo mengi katika sekta ya umiliki wa ardhi nchini lakini tunajaribu tuwezavyo kurekebisha. Mbeleni ilikuwa kwa kutoa hati za umiliki, lakini sasa tumerekebisha na tunawapa watu wengi nakala hizo,” akasema waziri huyo.

Visa vingine vilivyoripotiwa ni vya watu kupata mashamba yao yanamilikiwa na watu wengine, wakati hawajawahi kuuza, hali ambayo wabunge walilaumu maafisa katika wizara hiyo, kuwa ndio wanaendesha hila hizo.