Karua aanza mikutano ya kuvumisha Narc-K tayari kwa uchaguzi ujao

Karua aanza mikutano ya kuvumisha Narc-K tayari kwa uchaguzi ujao

Na STEVE NJUGUNA

KINARA wa Narc Kenya, Martha Karua ameanza ziara katika maeneo mbalimbali kote nchini ili kuvumisha chama hicho kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa mujibu wa Bi Karua, atakuwa akitembelea miji mbalimbali kukutana na wanachama wa Narc-K na baada ya mikutano hiyo, atatangaza mwelekeo atakaouchukua kuhusu kiongozi watakayempigia kura za urais.

“Kama kiongozi wa Narc Kenya, ninalenga kuandaa mikutano hii kuwasikiliza wanachama wetu na pia kuvumisha chama hiki kwa sababu tunalenga viti vingi zaidi katika uchaguzi wa Agosti,” akasema Bi Karua.

Alikuwa akizungumza mjini Nyahururu baada ya kukutana na wajumbe wa chama hicho kutoka eneobunge la Laikipia Mashariki.

Bi Karua pia alifichua kuwa Narc Kenya iko tayari kuingia kwenye miungano ya kisiasa na vyama vingine na hivi karibuni atatangaza wanasiasa anaotarajia kushirikiana nao.

“Lazima nishauriane na wanachama wangu pamoja na wajumbe wetu kupitia mikutano hii. Uamuzi wa nani wa kuungana naye au kutoungana naye utatolewa na uongozi wa chama chetu,” akasema Bi Karua.

Waziri huyo wa zamani pia alifichua kuwa tayari Narc Kenya imeandaa mikutano katika kaunti nne za Meru, Kirinyaga, Nyeri na Embu ambako wajumbe waliwaeleza kuhusu mkondo wa kisiasa wanaofaa kuchukua.

Aidha, mbunge huyo wa zamani wa Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga alikariri kuwa Narc Kenya itawasimamisha wagombeaji katika nafasi zote za uongozi.

Vilievile aliwataka Wakenya wasipige kura kwa msingi wa vyama bali falsafasa ya uongozi ya wawaniaji mbalimbali.

Pia aliwataka wanasiasa wa ukanda wa Mlima Kenya waungane kisha wawarai raia waelekeze kura zao kwenye mrengo ambao utapata ushindi.

“Kama viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya, tutafanya juu chini kuhakikisha kuwa watu wetu wanaungana na kuelekeza kura zao kwenye kapu moja. Tuachane na siasa za chuki na badala yake kila Mkenya aruhusiwe kuuza sera yake bila kuingiliwa wakati huu wa kampeni,” akaongeza Bi Karua.

  • Tags

You can share this post!

Githua: Gaspo tunahitaji taji la ligi kuu msimu huu

Kukubo, aliyeshika mkia 2007, atangaza kuwania urais tena...

T L