HabariSiasa

Karua adokeza kuungana na Mudavadi kuingia Ikulu 2022

June 5th, 2020 1 min read

NA ERIC MATARA

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya Bi Martha Karua amedokeza kuwa kuna uwezekano wa kuunda muungano wa kisiasa utakaojumuisha chama chake, kile cha Bw Musalia Mudavadi na vyama vingine vyenye maono sawa huku siasa za 2022 zikianza kupamba moto.

Bi Karua alisema Kenya inahitaji viongozi wenye fikra tofauti watakaonyanyua wananchi kutoka kwa masaibu yanayowakumba.

“Tumekuwa kwa mdahalo na chama cha ANC na viongozi wengine wenye maono sawa kuhusu kuunda muungano mmoja utaojizatiti kutatua changamoto zinazowaumiza wananchi.

“Tunahitaji viongozi wenye msukumo tofauti kufufua uchumi wetu ambao umeyumbishwa na mawimbi ya Covid-19, ili kuleta mazingira ya kuvutia wawekezaji nchini,” alisema Bi Karua kwenye mahojiano kwa runinga moja ya humu nchini.

Pia, kiongozi huyo alipuuzilia mbali juhudi za serikali za kutaka mabadiliko ya katiba, akisema taifa hili halihitaji kupiga kura ya maamuzi kuhusu katiba.

Alisema wazi kuwa atakuwa debeni kuchaguliwa Rais hapo 2022, hii ikiwa ni chini ya wiki moja tangu akutane na Bw Mudavadi, Peter Kenneth na Sally Kosgey.