Karua afufua Raila katika Mlima Kenya

Karua afufua Raila katika Mlima Kenya

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Narc Kenya, Martha Karua, ameleta mwamko mpya katika kampeni za Raila Odinga eneo la Mlima Kenya tangu kiongozi huyo wa ODM alipomteua kuwa mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wiki moja baada ya Bw Odinga kumteua, Bi Karua amefufua kampeni za Azimio kwa kuhutubia mikutano mfululizo katika kaunti sita za eneo la Mlima Kenya.

Katika mikutano hiyo, mwanasiasa huyo mwenye msimamo mkali amekuwa akiandamana na viongozi wanaounga Azimio ambao awali walikuwa wakiogopa kumuuza Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya, ambalo Naibu Rais William Ruto amejijengea umaarufu kwa zaidi ya miaka minne.

Licha ya kuwa ndani ya Azimio, viongozi hasa wa chama cha Jubilee na vyama vingine tanzu vya muungano huo walikuwa wakiogopa kuchapisha alama, ujumbe wa Azimio na picha ya Bw Odinga katika mabango ya kampeni kwa kile walisema ni kutiwa baridi na umaarufu wa Dkt Ruto na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Hata hivyo, ndani ya wiki moja, Bi Karua amezunguka kaunti za Kirinyaga, Nyeri, Embu, Meru, Tharaka Nithi, Murang’a na Kiambu katika kile alichotaja kama ziara ya kusalimia wapigakura.

Miongoni mwa wanasiasa ambao uteuzi wake uliwapa nguvu ya kushiriki kampeni za Bw Odinga mlimani ni katibu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni, aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando, mbunge wa bunge la Afrika Mashariki Mpuri Aburi na Waziri wa Kilimo Peter Munya.

Wengine ambao wamepata ujasiri wa kumfanyia kampeni Bw Odinga ni Waziri wa Utumishi wa Umma, Profesa Margaret Kobia, Waziri wa Habari na Mawasiliano Joe Mucheru, Mbunge wa Kieni Kanini Kega na Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Murang’a Sabina Chege.

“Uteuzi wa Bi Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga ndani ya Azimio uliwapa viongozi wa Mlima Kenya mwelekeo ambao walikuwa wamekosa. Hii ndiyo sababu mwamko mpya unashuhudiwa katika kampeni za Azimio eneo la Mlima Kenya. Jeshi la Bw Odinga eneo hilo limepata jemedari,” asema mchambuzi wa siasa Bw Isaac Gichuki.

Anasema mwamko ambao Bi Karua amezua eneo hilo umetisha kampeni ya Dkt Ruto, ambaye pia amekita kambi katika eneo hilo tangu Bi Karua alipoteuliwa na Bw Odinga.

MOJA KWA MOJA

Leo Jumatatu Dkt Ruto anatarajiwa kuendelea na kampeni zake katika maeneo ya Kangema na Mathioya, Kaunti ya Murang’a.

Akiwa Nyeri Jumamosi, Dkt Ruto na washirika wake walimtaka Bw Odinga kuwakabili moja kwa moja badala ya kumtumia Bi Karua.

“Hatutamshambulia dada yetu lakini tutakabiliana na Raila hadi astaafu siasa,” alisema Rigathi Gachagua, mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto.

Alikuwa akiwasilisha ujumbe huo katika mikutano aliyohutubia maeneo tofauti kwa siku sita mfululizo.

Katika mikutano hiyo, viongozi waliokuwa wakiepuka kuandaa mikutano ya hadhara katika eneo hilo kupigia debe Bw Odinga wakiwemo mawaziri, walionekana kuwa na ujasiri wa kumvumisha kiongozi huyo wa ODM kama anayefaa kuwa rais wa tano wa Kenya.

Katika ujumbe wake kwa wakazi wa Mlima Kenya, Bi Karua alisisitiza kuwa ni Bw Odinga anayeweza kuleta mageuzi ya dhati nchini kwa manufaa ya raia na kupigana na ufisadi.

“Mnaelewa mimi ni mchapa kazi, mkituona katika timu ya Raila mjue kuwa tuko na wachapa kazi,” alisema akiwa Embu.

Uteuzi wa Bi Karua ulipokolewa vyema katika maeneo mengi ya nchi hasa kutokana na rekodi yake ya kutetea utawala wa kisheria na heshima kwa Katiba.

Pia suala la kuwa mwanamke limefurahiwa na makundi ya kutetea haki za kijinsia, wakisema uteuzi wake ni hatua kubwa katika ustawi wa demokrasia nchini.

  • Tags

You can share this post!

Washirika wa Raila Magharibi wamrai Kalonzo kurudi Azimio

Kalonzo kuamua leo ikiwa ama atawania au atarejea Azimio

T L