Habari MsetoSiasa

Karua ala hu baada ya korti kuamuru Waiguru hakuiba kura

December 20th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

OMBI la mwanasiasa maarufu Martha Wangari Karua  la kutaka ushindi wa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ufutiliwe mbali umekataliwa tena Alhamisi.

Hii ni baada ya Mahakama ya Rufaa kusema kuwa ombi la Karua halikuwa na msingi wowote wa kuweza kubatilishwa kwa ushindi wa gavana Waiguru.

Bi Karua, ambaye ni kiongozi wa chama cha Narc Kenya alikuwa amedai kuwa ushindi wa Bi Waiguru katika uchaguzi mkuu wa 2017 ulichangiwa na wizi wa kura na aina nyinginezo za udaganyifu.

Kabla ya uamuzi huo kutolewa Bw Karua ambaye ni waziri wa zamani wa Haki na Masuala ya Kikatiba alituma ujumbe kupitia Twitter akiahidi kuheshimu uamuzi wa kesi hiyo.

“Niko kortini nikisubiri uamuzi wa kesi yangu ya rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi. Nitaheshimu uamuzi wa korti, na ikiwezekana nitafuata mkondo uliopo kusaka haki,” akasema huku akionekana kubashiri matokeo ya kesi hiyo.

Hata hivyo,  mwanasiasa huyu mkongwe ameelekea katika Mahakama ya Juu, kupinga uamuzi uliotolewa Alhamisi.