Karua alazimisha Ruto kufanya hesabu upya

Karua alazimisha Ruto kufanya hesabu upya

NA BENSON MATHEKA

MUUNGANO wa Kenya Kwanza Alliance, unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, utalazimika kupanga upya mikakati yake baada ya uteuzi wa Kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua kuwa mwaniaji mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya kukoroga mipango yao.

Siku moja baada ya Bi Karua kukubali wadhifa huo, baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza Alliance wanaonya kuwa Azimio itawaonyesha kivumbi kwenye kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 wasipojipanga upya.

Kiongozi wa chama cha Tujibebe Wakenya, William Kabogo anakiri kwamba uteuzi wa Bi Karua utawatoa kwenye kampeni hasa katika eneo la Mlima Kenya: “Kenya Kwanza tunafaa kujiandaa kwa kampeni kali.”

Wachanganuzi wa siasa wanasema onyo la Bw Kabogo linatokana na nguvu ambazo kampeni ya Azimio imepata baada ya Bi Karua kutangazwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

“Mikakati ya Kenya Kwanza, na hasa mgombea urais wao Naibu Rais William Ruto imetikiswa na ujio wa Karua kama mgombea mwenza wa Bw Odinga. Hii ni ikizingatiwa kuwa akiwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa katika wadhifa huo anaweza kuzoa kura nyingi za wanawake kote nchini,” akasema mchanganuzi wa siasa Meshack Owour.

Anasema hata ingawa Dkt Ruto ameteua mgombea mwenza kutoka eneo la Mlima Kenya anakotoka pia Bi Karua, maadili ya kiongozi huyo wa Narc-Kenya yanaweza kubadilisha wimbi la kisiasa na kuimarisha umaarufu wa Bw Odinga kote nchini

“Karua sio tu kiongozi wa eneo la Mlima Kenya, mbali anatambuliwa kote nchini. Ikiwa wapiga kura watazingatia maadili na tabia ya mwaniaji, basi umaarufu wa Azimio katika ngome za Kenya Kwanza utaongezeka kwa kuwa Karua hajahusishwa na ufisadi na anapenda kufuata sheria kikamilifu,” akasema Bw Owuor.

Anasema mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua anaweza kuwa mfanyabiashara stadi na mwenye ulimi mtamu, lakini maadili yake tayari yametiwa doa na kesi zinazomkabili kortini kwa madai ya ufisadi wa mabilioni ya pesa.

Akizungumza katika runinga ya Citizen mnamo Jumatatu usiku, Bi Karua alisema hatayumba katika msimamo wake hata akiwa katika serikali.

“Kila kitu lazima kifanywe kwa misingi ya Katiba na sheria. Nawahakikishia Wakenya kwamba utawala wa sheria lazima utazingatiwa,” akasema.

MSISIMKO MPYA

Kulingana na mchanganuzi wa siasa na uchaguzi Thomas Maosa, tikiti ya Bw Raila na Bi Karua imetatiza kwa kiwango kikubwa mikakati ya Kenya Kwanza.

“Karua ameleta msisimko mpya kwenye kampeni za uchaguzi mkuu. Msisimko huu utadumu ikizingatiwa ni siku 80 tu kabla ya uchaguzi,” akasema Bw Maosa.

Anasema kwa kawaida wapigakura wengi na hasa wanawake wanataka kuwa sehemu ya historia ilivyofanyika katika uchaguzi mkuu wa Amerika, Joe Biden alipomteua Khamala Harris kuwa mgombea mwenza wake.

“Kuanzia sasa kuelekea uchaguzi mkuu, kutakuwa na wimbi jipya. Kampeni zitabadilika kuwa kuhusu maadili, utawala wa sheria na haki za wanawake na usawa,” asema.

Bw Maosa anasema kibarua cha Azimio kitakuwa ni kudumisha msisimko ambao uteuzi wa Bi Karua umezua kote nchini.

Hata hivyo, kulingana na mchanganuzi wa siasa Geff Kamwanah, itakuwa kibarua kigumu kubomoa mtandao wa umaarufu ambao Dkt Ruto amejenga kwa zaidi ya miaka minne ambayo amekuwa akifanya kampeni.

“Ni kweli uteuzi wa Karua umezua msisimko lakini ni muhimu kukumbuka kuwa Dkt Ruto amekuwa katika kampeni kwa miaka minne na amejenga umaarufu kupitia ahadi yake ya kusaidia maskini,” asema Bw Kamwanah.

  • Tags

You can share this post!

Amerika kupeleka tena wanajeshi wake Somalia

TAHARIRI: Nchi itanawiri zaidi tukiwapa wanawake nafasi

T L