Karua apendekeza wakati wa uchaguzi kuwe na maafisa maalum

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua amesema mvutano unaoshuhudiwa mara kwa mara wakati wa chaguzi kuu nchini, utasuluhishwa endapo kutakuwa na maafisa maalum watakaokuwa wakifuatilia shughuli zote bila ushawishi wowote.

Bi Karua amesema maafisa hao hawapaswi kutoka katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wala kuhusishwa na siasa.

“Wawe maafisa wa kipekee watakaokuwa wakishirikiana na IEBC wakati wa uchaguzi. Kazi yao iwe kufuatilia zoezi zima, upigaji kura unapoendelea, wakati wa kuhesabu wawe ange na kujiri na matokeo yao,” wakili Karua akapendekeza.

Alisema wanapaswa kuwa huru, na wasioripoti kwa asasi yoyote ile. “Mfumo huu ukitekelezwa, hakuna atakayelalamikia udanganyifu na wizi wa kura. Matokeo yao baadaye yatalinganishwa na ya IEBC,” Waziri huyo wa zamani wa Masuala ya Haki na Katiba akafafanua.

Bi Karua alisema kesi za uchaguzi zinazowasilishwa mahakamani huenda zikapungua au hata zikawa historia.

Kila mwaka wa uchaguzi mkuu, idara ya mahakama hupokea malalamishi ya udanganyifu kusakatwa, hasa kutoka kwa wagombea waliobwagwa. Visa vya wizi wa kura vimekuwa vikiripotiwa.