Karua apiga jeki wawaniaji wa kike – Utafiti

Karua apiga jeki wawaniaji wa kike – Utafiti

NA CHARLES WASONGA

KUTEULIWA kwa kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kumechochea kuimarika kwa umaarufu wanawake wanaowania ugavana katika kaunti nne nchini.

Matokeo ya kura ya maoni yaliyofanywa kati ya Mei 16 na Mei 23 katika kaunti za Homa Bay, Nakuru, Embu na Kilifi yalionyesha idadi kubwa ya wapiga kura wanaunga mkono wawaniaji wa kike.

Bi Gladys Wanga amempiku aliyekuwa gavana wa Nairobi Evans Kidero kwa kuandikisha umaarufu wa kiwango cha asilimia 57.9 dhidi ya asilimia 38.3, kulingana na utafiti huo ulioendeshwa na Shirika la Consortium of Researchers on Governance Africa (CORG-Afrika).

Katika Kaunti ya Nakuru, Seneta Susan Kihika anakaribiana na Gavana Lee Kinyanjui kwa umaarufu kwa kuungwa mkono na asilimia 37.5 ya wapiga kura.

Gavana Kinyanjui ndiye aliongoza kwa kuandikisha umaarufu wa asilimia 39.4, akitetea kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee.

Hali ni sawa na hiyo katika Kaunti ya Kilifi ambapo Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa anamkaribia aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Ardhi Gideon Mung’aro.

Bi Jumwa anayewania kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) aliandikisha umaarufu wa 38.7 huku Bw Mung’aro anayewania kwa ODM akiwa mbele kwa kupata asilimia 43.7.

Na katika kaunti ya Embu, mbunge maalum Cecily Mbarire aliandikisha umaarufu wa asilimia 32.6 nyuma ya Bw Lenny Kivuti ambaye anaongoza kwa kuungwa mkono na asilimia 41.2 ya wapiga kura.

“Licha ya Bw Kivuti kuonekana mbele ya Bi Mbarire, umaarufu wa mbunge huyo maalum umeimarika kutoka asilimia 28 aliyoandikisha mnamo Machi 20,” akasema mkurugenzi mkuu wa CORG-Africa Charles Mc’ Olonde.

Kuhusu Homa Bay, Bw Mc’Olonde alisema matokeo hayo ni tofauti yale ya mwezi huo wa Machi ambapo Dkt Kidero aliongoza kwa umaarufu.

“Katika matokeo ya utafiti wetu Machi 20, mwaka huu, Bi Wanga alikuwa nyuma kwa umaarufu wa asilimia 30 huku Kidero alikuwa juu kwa asilimia 44. Tunaamini kuwa matokeo ya sasa yamechochewa na wimbi la uteuzi wa Bi Karua kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga,” akawaambia wanahabari.

“Tunaaamini kuwa hali hiyo imechochewa na hatua ya mgombea wa Azimio Raila Odinga ya kumteua Bi Karua kuwa mgombea mwenza wake,” Bw Mc’Olonde akaongeza.

Bi Wanga anawania kwa tiketi ya ODM ilhali Dkt Kidero anawania kama mgombeaji wa kujitegemea katika eneo hilo ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Odinga.

Bw Mc’ Olendo alisema kuwa jinsia ni mojawapo ya masuala ambayo walizingatia walipokuwa wakiwahoji wapiga kura katika kaunti hizo nne.

Masuala mengine yaliyozingatiwa katika utafiti huo ni muegemeo wa vyama, manifesto ya wawaniaji, maadili na mikakati ya kampeni.

  • Tags

You can share this post!

Akita kwa kilimo mseto baada ya kuacha ualimu

TUSIJE TUKASAHAU: Rais Kenyatta asisahau serikali yake...

T L