Siasa

Karua apuuza ‘madharau ndogondogo’ ya Kalonzo kusema hatoshi mboga

March 22nd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua, Ijumaa alipuuzilia mbali kauli ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwamba hatoshi mboga kuuongoza mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Kwenye ujumbe alioandika katika mtandao wa X (zamani ukiitwa Twitter), Bi Karua alisema wapigakura ndio watakaoamua kuhusu kiongozi watakayemchagua uchaguzi utakapofika.

Kauli ya Bi Karua inafuatia taarifa iliyochapishwa na gazeti la Taifa Leo, Ijumaa, ambapo Bw Musyoka alisema kuwa kiongozi huyo hajatimiza vigezo vya kuuongoza mrengo huo, ikiwa kiongozi wake-Raila Odinga-atachaguliwa kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

“Ushauri wangu kwa ndugu yangu, Kalonzo Musyoka, ni kwamba anafaa kuangazia juhudi za kujiuza kwa Wakenya, na kuacha wapigakura kuamua kuhusu kiongozi anayefaa zaidi,”akasema.

Kwenye taarifa hiyo, Bw Musyoka alisema kuwa ndiye kiongozi bora kuchukua uongozi wa mrengo huo, ikiwa Bw Odinga atachguliwa kama mwenyekiti wa AUC.

Taarifa hiyo pia iliangazia mgawanyiko uliopo katika muungano huo, kuhusu ni nani atakayekuwa mpeperusha bendera wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Musyoka ameteuliwa mara mbili na Bw Odinga kuwa mgombea—mwenza wake; kwenye chaguzi kuu za 2013 na 2017. Hata hivyo, Bw Odinga alimteua Bi Karua kuwa mgombea-mwenza wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Tangu Januari, Bw Musyoka amekuwa akiendesha kampeni katika sehemu tofauti nchini, huku akisistiza kuwa ndiye atakayekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Azimio 2027.

Ni hali ambayo imezua maswali kuhusu mwelekeo atakaochukua Bi Karua, kwani hajakuwa akionekana kushiriki sana katika masuala yanayohusu muungano huo.

Azimio, hata hivyo, imekuwa ikikanusha kuhusu uwepo wa migawanyiko yoyote ya kisiasa.

Mwaka uliopita, Bw Musyoka alisema kwamba ikiwa hatakuwa debeni 2027,  basi hilo linamaanisha atastaafu kutoka ulingo wa siasa.

“Ikiwa nitashinikizwa kumwachia Raila nafasi ya kuwania urais, basi hilo linamaanisha nitaenda nyumbani. Sitakubali kutupilia mbali nia yangu ya kuwania urais. Wakenya wanasema hivyo. Wakati huu, (Rais William Ruto) anafaa kuwa tayari,” akasema.

Bw Musyoka pia ametangaza mikutano ambayo amekuwa akifanya kama “matayarisho ya mapema kwa uchaguzi mkuu wa 2027”.

Viongozi wa Wiper wamekuwa wakisisitiza kuwa ndiye kiongozi bora kuwania urais.

Wiki hii, kiongozi huyo alielekeza kampeni zake katika Kaunti ya Kisii, alikofungua afisi za chama chake na kuzindua shughuli za kuwasajili wanachama, ili kukipa nguvu zaidi.