Habari MsetoSiasa

Karua atakiwa kushirikiana na Waiguru

June 19th, 2018 1 min read

Na KNA

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua ameraiwa kukubali uamuzi wa mahakama kwamba Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru alichaguliwa kihalali.

Mahakama Kuu ya Kerugoya iliamua kwamba Bi Waiguru alichaguliwa bila matatizo yoyote, hivyo kutupilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na Bi Karua kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na makosa.

Kwa hayo, diwani wa wadi ya Central, Imam Abdi alimwomba Bi Karua kuheshimu uamuzi wa wakazi wa kaunti hiyo, kwa kuungana na Bi Waiguru kuwahudumia pamoja.

Bw Rahman alisema kwamba watu wengi katika kaunti hiyo, wanaona kesi ya Bi Karua kama kuwapotezea muda.

“Wakazi wengi wa Kirinyaga wanataka maendeleo kwa sasa, si kesi zisizoisha,” akasema.

Akaongeza: “Tumechoshwa na mvutano kati ya viongozi hawa, ndipo tunamwomba Bi Karua kuondoa mpango wa kwenda katika Mahakama ya Rufaa.”

Aliwaomba wawili hao kuungana kwa maslahi ya ustawi wa kiuchumi ya kaunti hiyo.

“Tunamfahamu Bi Karua kama kiongozi shupavu ambaye anaweza kuchangia sana katika masuala ya maendeleo. Tunauomba uongozi wa kaunti kumshirikisha katika maamuzi muhimu yanayohusu uongozi wake,” akasema.

Wawili hao wamekuwa katika vita vikali vya kisiasa, ambapo Bi Ngirici amekuwa akiendesha miradi yake ya maendeleo kupitia kundi la Ngirici Rescue Team, ambako amekuwa akimlaumu Bi Waiguru kwa kutotimiza ahadi alizotoa kwa wakazi.

Katika kesi ya Bi Karua, juhudi za Bi Waiguru kuisimamisha mahakama ziligonga mwamba, mahakama ikishikilia kwamba ni haki ya mlalamishi katika kesi hiyo kusikilizwa tena.

Masaibu hayo yanamtokea Bi Waiguru aliyechaguliwa kama gavana baada ya kulazimika kujiuzulu hapo awali kama Waziri wa Ugatuzi katika Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kutokana na sakata ya madai ya ufisadi katika Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS).

Katika sakata hiyo, inakisiwa kwamba karibu Sh791 milioni zilipotea katika hali tatanishi, ila Bi Waiguru amekuwa akishikilia kuwa hakuhusika kwa vyovyote vile.