NA LEONARD ONYANGO
KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi na mwenzake wa Narc Kenya, Martha Karua ndio wanapendelewa na Wakenya kuwa manaibu wa wawaniaji wakuu wa urais.
Ripoti ya utafiti wa kura ya maoni uliodhaminiwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG), unaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanapendelea Bw Mudavadi kuwa mwaniaji mwenza wa Naibu wa Rais William Ruto.
Bw Mudavadi anaongoza kwa asilimia 19, Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki anafuatia kwa asilimia 14, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru (asilimia 13), Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi (asilimia 9), Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua (asilimia 8) na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro (asilimia 4).
Seneta wa Nakuru Susan Kihika, mbunge wa Kandara Alice Wahome, Gavana wa Machakos Alfred Mutua, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula wote wana chini ya asilimia 2.
Uwezekano wa Bw Mudavadi kuteuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto, hata hivyo, ni finyu, kwani mkataba wa makubaliano miongoni mwa vigogo wa Kenya Kwanza unasema kuwa mwaniaji wa urais na mwaniaji mwenza atatoka katika chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Dkt Ruto.
Hiyo inamaanisha kuwa Prof Kindiki huenda akateuliwa kuwa mwaniaji mwenza iwapo Naibu wa Rais atazingatia umaarufu.
Kwa upande wa Azimio La Umoja – One Kenya, asilimia 41 ya Wakenya wanataka Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.
Bi Karua anapendelewa zaidi katika maeneo ya Pwani, Kaskazini Mashariki, Kati, Nyanza, Bonde la Ufa, Magharibi, Nyanza na Nairobi.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye anafuatia kwa asilimia 27 anaungwa mkono na idadi kubwa ya wakazi wa eneo la Mashariki kwa asilimia 57.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Infotrak Research & Consulting, unaonyesha kuwa aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Sabina Chege, Waziri wa Kilimo Peter Munya na magavana Hassan Joho (Mombasa), Charity Ngilu (Kitui) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) kila mmoja amepata chini ya asilimia 10.
Jopo lililoteuliwa na Bw Odinga kumtafutia mwaniaji mwenza mnamo Alhamisi lilimkabidhi orodha ya watu watatu ambao atateua mmoja kuwa ‘naibu’ wake.
Mkuu wa jopo hilo Bw Noah Wekesa alisema kuwa majina hayo yamepangwa kwa kuzingatia alama ambazo kila mhojiwa alipata.
Japo Bw Wekesa alikataa kufichua majina ya watu hao, Taifa Leo imebaini kuwa bahasha hiyo inajumuisha majina ya Bi Karua, Bw Kalonzo na Bw Kenneth.
Bw Odinga anatarajiwa kutangaza mwaniaji mwenza wake kabla ya Jumatatu wiki ijayo, ambayo ni siku ya mwisho kwa wawaniaji wa urais na ugavana kupeleka majina yao pamoja na wagombea wenza wao kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Matokeo ya utafiti huu huenda yakaongeza shinikizo kutoka eneo la Mlima Kenya kutaka Bw Odinga kumteua Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wake.
Utafiti huo unaonyesha kuwa Bi Karua anaungwa mkono na idadi kubwa ya wanawake kwa asilimia 42 ikilinganishwa na asilimia 40 ya wanaume.