Habari

Karua sasa amlaumu Uhuru

June 29th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua amemsuta Rais Uhuru Kenyatta kwa kile anachodai ni kuwatelekeza watu wa Kirinyaga licha ya kuwepo kwa ushahidi kuwa kaunti hiyo inazongwa na usimamizi mbaya.

“Inaonekana kuwa Rais hajali kwamba Gavana Anne Waiguru na washirika wake wanapora mali ya Kirinyaga. Maseneta wa Jubilee walikuwa mstari wa mbele kumtakasa Waiguru licha ya ushahidi kuonyesha kuwa alihusika na ufisadi,” akasema.

Akihojiwa katika kituo cha runinga cha Citizen Jumatatu asubuhi, Bi Karua ameonya kuwa endapo Rais Kenyatta hataingilia kati suala hilo ambalo limeibua uhasama baina ya madiwani na Gavana Waiguru, wakazi wa Kirinyaga watakuwa katika masaibu tele.

Karua ambaye aligombea akashindwa na Waiguru katika kinyang’anyiro cha ugavana 2017 vilevile alidai kuwa wanachama wa kamati maalum iliyochunguza tuhuma dhidi ya Waiguru walipokea simu kutoka kwa watu fulani wakiwataka wasimhusishe gavana huyo na makosa hayo.

“Ningependa kusema wazi kwamba wanachama wa kamati hiyo walipokea simu. Tunafahamu kwamba kulikuwa na mikutano ya usiku; tunafahamu Spika alipigiwa siku na habari hizo tulipewa na maseneta ambao hawakutaka kutajwa,” akasema.

Akaongeza: “Kulikuwa na ushahidi tosha kwamba zabuni zilipeanwa kinyume cha sheria na maseneta pia walikiri watu wasiohitimu waliajiriwa. Kwa mtazamo wangu hayo ni makosa ambayo yana uzito wa kuwa msingi wa kuondolewa kwa gavana mamlakani,” Bi Karua akasema.

Mnamo Ijumaa, Kamati maalum ya Seneti iliyochunguza tuhuma kwenye hoja ya kumwondoa afisini Bi Waiguru ilimwondolea lawama.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Cleophas Malala (Seneta wa Kakamega) alisema Bunge la Kaunti ya Kirinyaga halikufafanua tuhuma za ukiukaji wa Katiba, matumizi mabaya ya afisi na ufisadi, ambazo gavana huyo alihusishwa nazo.

“Baada ya kamati hii kuchunguza suala hili, kulingana na sehemu ya 33 na sheria za seneti nambari 75 (2) imebainika kuwa mashtaka mawili dhidi ya gavana hayakufafanuliwa,” akasema Bw Malala.