Makala

KASHESHE: Agomea shoo Saudia

July 12th, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

NYOTA wa hip hop kutoka Amerika, Nicki Minaj, kafutilia mbali shoo yake iliyokuwa imeratibiwa kufanyika Saudi Arabia kutokana na sheria kali za kibaguzi kwa wanawake, watu wenye uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.

Staa huyo ni miongoni mwa mastaa kibao walioratibiwa kutumbuiza nchini humo katika tamasha kubwa ya Jeddah World Fest itakalofanyika Julai 18.

Hata hivyo Nicki kasema hataweza kutumbuiza licha ya kupokea mwaliko kwa sababu nafsi yake haiwezi kumruhusu kupiga shoo katika taifa ambalo lina sheria kibao zinazokiuka haki za kibinadamu.

“Baada ya kuwaza sana nimeamua siwezi kuendelea na ratiba yangu ya shoo kule Jeddah World Fest. Ijapokuwa ningelipenda sana kuwaletea mashabiki wangu wa Saudi Arabia shoo nyumbani, nimeshindwa baada ya kupevuliwa kuhusu sheria tata zilizopo huko. Napenda kuona haki za wanawake na watu wenye uhusiano wa jinsia moja zikiheshimiwa, na pia uhuru wa kujieleza,” Minaj alitoa taarifa.