Makala

KASHESHE: Burna Boy amwaga povu kali

September 6th, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

UVAMIZI na mauaji yanayoendelea Afrika Kusini yakilenga wasio wazalendo yamepelekea kuzuka kwa bifu mbaya kati ya nyota wa muziki kutoka Nigeria Burna Boy na AKA wa Afrika Kusini.

Miongoni mwa wanaolengwa kwenye uvamizi huo ni raia wa Nigeria. Sasa kutokana na matukio hayo, Burna Boy kasisitiza kutowahi kukanyaga Afrika Kusini.

“Sijatia mguu SA toka 2017 na sitawahi mpaka siku ambayo serikali ya Afrika Kusini itakapofanikiwa kutatua ubaguzi unaoendelea,” katupia.

Lakini hata zaidi ishu hiyo ilimsukuma kuingia kwenye bifu na rapa AKA. AKA amekuwa akijitahidi kuposti jumbe za mariadhiano na mara kwa mara akitumia utani kuhimiza umoja na amani.

Hata hivyo jumbe zake ziliishia kumchefua Burna Boy ambaye katishia kumdhuru sehemu yeyote watakayokutana akimtahadharisha kuwa bora awe akiandamana na ulinzi wa kutosha muda wote.

Huku hayo yakijiri, naye Tiwa Savage kaamua kufutilia mbali shoo yake iliyokuwa imeratibiwa kufanyika mjini Johannesburg akisisitiza kuwa hawezi kutumbuiza katika taifa ambalo wazalendo wenza wanadhulumiwa na kuhangaishwa.