Makala

KASHESHE: Covid-19 yatia breki fungate

March 20th, 2020 1 min read

Na THOMAS MATIKO

MWANAMUZIKI wa bendi ya Sauti Sol, Bien Baraza kalazimika kuahirisha fungate yake na mkewe Chiki Kuruka kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona.

Wawili hao walifunga ndoa yao wiki mbili zilizopita katika mtaa wa kifahari wa Lavington. Ilikuwa ni sherehe ya ukimya huku wageni wapatao 150 wakialikwa.

Sherehe hiyo ilikuwa ni ya kusherehekea upatanisho wa wawili hao kama mke na mume ambapo awali walifunga ndoa rasmi kwenye afisi za mwanasheria mkuu.

Na huku wakiwa wameanza harakati za kwenda fungate, sasa wamelazimika kukanyagia kutokana na mkurupuko huo ambao umefanya mataifa mbalimbali kuzuia wananchi wasio wazalendo kuingia katika nchi zao.

Hata hivyo Bien anasema hali itakapotulia bado watakwenda tu fungate yao.

“Ikitokea tuende, nafikiri sehemu ambayo nitapendelea zaidi kwenda kwa ajili ya fungate ni hapa hapa tu barani Afrika,” akasema.

Bien na Chiki waliamua kuhalalisha mahusiano yao baada ya kuishi kama ‘mke na mume’ kwa muda wa miaka sita.