Makala

KASHESHE: Erico afunguka kuhusu penzi lake na Maribe

November 15th, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

MVUNJA mbavu maarufu Eric Omondi kafunguka namna mambo yalivyotokea hadi akaishia kumpachika ujauzito mtangazaji wa zamani wa runinga Jacque Maribe.

Uhusiano wao ulidumu kwa kipindi kifupi sana lakini ukaishia kuwajalia na mtoto wa kiume mwenye miaka minne ambaye hivi majuzi waliamua kumaliza uvumi kwa kuthibitisha kwamba walizaa pamoja baada ya kufanya siri kwa miaka kadhaa.

Akitoa ya moyoni, Erico alisema kafahamiana na Maribe kwa miaka mingi sana ambapo walianzisha uhusiano wa kirafiki hadi ukaishia kwa wao kujifunika shuka moja kabla ya kutemana. Na hata baada ya kutemana, waliamua kudumisha urafiki wao ambao upo mpaka sasa.

“Tulikutana na Jacque Maribe akiwa anafanya kazi Kiss TV kama ripota na mimi nikiwa mchekeshaji mtangazaji pale Radio Jambo. Tuliishia kuwa marafiki wakubwa sana baada ya kwenda deti yetu ya kwanza Java iliyopo pale Sarit Center. Tukaahidiana kwa lolote lile tutadumisha urafiki wetu hadi kifo.

“Hata baada yangu kuondoka Radio Jambo na yeye akaenda Citizen tumeendeleza urafiki wetu mpaka leo hii,” Omondi kasimulia.

Kauli yake imetoka kipindi kukiwa na madai kwamba huenda wawili hao wamerudiana toka walipoamua kuweka wazi kwamba walizaa pamoja na kisha kuanza kuonekana wakila bata pamoja na mwanao Zahari.