Makala

KASHESHE: Lupita na wenzake mashakani

May 31st, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

MWIGIZAJI staa wa hapa nyumbani anayevuruga kule Hollywood Lupita Nyong’o pamoja na timu yake nzima iliyohusika kwenye utengenezaji wa filamu kubwa Black Panther wameshtakiwa.

Bodi ya turathi za kitaifa nchini Ghana (The Ghana National Folklore) imeamua kuanzisha kesi dhidi ya kampuni ya Marvel Studios iliyohusika kwenye utengenezaji wa filamu hiyo iliyojumulisha Waafrika tupu kwa asilimia kubwa.

Malalamishi ya bodi hiyo ni kwamba kina Lupita waliamua kutumia vazi la kiasili la Ghana, lifahamikalo kama ‘Kente’ pasi na kupata idhini kamili.

Bodi hiyo inadai kuwa, chini ya sheria za hatimiliki, Marvel ilistahili kuomba ruhusa kutoka kwao kabla ya kuchukua uamuzi wa kutumia ‘Kente’ katika filamu hiyo iliyoishia kuvunja rekodi kwa kuingiza dola 1.344 bilioni kufikia Mei 22, 2018.

Bodi hiyo inasisitiza kuwa inataka kulipiwa fidia lau sivyo itabidi tu wakutane mahakamani.