Makala

KASHESHE: Masaibu ya Mbosso

September 20th, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

NYOTA wa Bongo Flava, Mbosso kasema kuwa hakushtushwa na hatua ya familia ya mpenzi wake wa zamani marehemu Boss Martha kumruka kwenye suala la kuzaa naye.

Mbosso alidhalilishwa waziwazi kwenye mazishi ya mcheshi huyo siku chache zilizopita kwa kuzuiwa kuingia kwenye eneo la maziko.

Lakini hata zaidi wakati wa kusoma wasifu wa marehemu, familia ilikana kuwa alikuwa na mtoto.

Mbosso na Martha walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa miaka mitano ila walishindwa kuwa pamoja kutokana na pingamizi kutoka kwa familia ya marehemu ambayo ni ya Kikristo na yeye ni Mwislamu.

Kwa kipindi hicho walichokuwa pamoja, walijaliwa kumpata mtoto wa kiume mwenye miaka minne.

Hata hivyo kwenye mazishi hayo, familia ya Boss Martha ilikana kuwa marehemu alikuwa na mtoto.

Lakini pia Mbosso alipojaribu kuhudhuria, alizuiwa na familia hiyo.

Familia

Akifunguka kuhusu suala hilo, Mbosso kasema sio mara ya kwanza mambo kama hayo yanamkuta kwani hata Martha akiwa uhai, familia yake haikuwahi kumpenda.

“Kitendo cha kunikana si kipya na nilitarajia watafanya hivyo kwa sababu walisha nikana siku nyingi,” Mbosso alisema kwenye mahojiano ya hivi majuzi na chombo kimoja cha habari kule Tanzania.

Boss Martha aliyekuwa mchekeshaji, alifariki dunia Jumatano ya wiki iliyopita baada ya kuugua homa kali iliyosababishwa na maumivu ya uti wa mgongo.