Makala

KASHESHE: Mejja sasa ana kiosha roho

August 23rd, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

MIEZI michache tu baada ya kufichua kuwa mke wake alimkimbia pasi na sababu, Mejja – rapa maarufu wa kundi la The Kansoul – kampata mpenzi mwingine.

Majuzi alitupia picha yake akiwa na kidosho huyo na safu hii ilipomcheki, alithibitisha kuwa kweli ndiye mpenzi wake mpya.

Julai 2019 alifichua kuwa nusura ajitie kitanzi baada ya kuachwa na mkewe kwa mataa.

Hadi anatemwa, walikuwa wamedumu kwenye ndoa kwa miaka mitano na kujaliwa binti mmoja.

Mejja alifichua kwamba alipata ujumbe kutoka kwa mkewe kipindi akiwa amekwenda kwenye shoo, akimfahamisha kuwa waachane.

Aliporudi nyumbani, alimkuta tayari kaondoka.

Nyota huyo anasisitiza kuwa mpaka leo hafahamu sababu yake kuondoka sababu hawakuwa wamekorofishana.

Ishu hiyo ilimsababishia msongo wa mawazo na hata kumfanya kutaka kujitia kitanzi kwani pia alimwacha kipindi akiwa ametoka hospitalini kufanyiwa operesheni ya kidoletumbo (appendix).