Makala

KASHESHE: Naandamwa na mafisi tu!

April 26th, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

MWANAMUZIKI wa kike Victoria Kimani kafichua kuwa anatamani sana kuolewa na kujaliwa watoto ila tatizo ni kuwa wanaume wengi wanaomtokea ni mafisi.

Kichuna huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa sasa, kawa singo kwa muda wa miaka miwili sasa toka alipotemana na mpenziwe wa zamani Mnigeria Stanely Obiamulu aishiye Afrika Kusini.

Toka kipindi hicho Kimani kawa singo na ijapo amekiri kutamani kumpata mpenzi, imekuwa shughuli.

“Kuna mwanamume ninayemzimikia kishenzi na ningetamani kutoka naye, ila nafikiri yeye hapendi kuwa na mimi. Maisha yangu ya mahusiano ndio kama hivyo yamekufa zamani,” alitanguliza kusema.

“Hata hivyo, natamani sana kuwa na familia, nimlee mwanangu katika nyumba iliyo na baba sababu maisha ya kuwa singo mama siwezi, nitachizi. Ila sasa tatizo ni kwamba sijampata mwanaume kamili, wengi hawa waongo tu. Wanakuwa sio wakweli na maisha yao. Hivyo nipo radhi kusubiri hadi nitakapompata yule tutakayesitiriana maisha,” alisema.

Pamoja na yote, Victoria kasisitiza kuwa kamwe hawezi kutoka na mwanamume asiye na hela lakini hata zaidi asiye na akili za kibiashara.