Makala

KASHESHE: Nadia ayapa kisogo mapenzi

June 26th, 2020 1 min read

Na THOMAS MATIKO

MWANAMUZIKI Nadia Mukami kachorea masuala ya mahusiano kwa sasa ili kujenga taaluma yake.

Msupa huyo mwenye umri wa miaka 23 kasema amegundua kuwa umri alionao kwa sasa ni wa kujenga taaluma yake ya muziki mwanzo kabla ya kuwazia mahusiano.

Anasema kuwa mwanamuziki wa kike na kuwepo kwenye mahusiano kwa wakati huo huo kutavuruga azma yake ya kujijengea taaluma ya kufana.

Lakini hata zaidi anasema, kwa sasa hana mpango wa kuwa kwenye mahusiano baada ya kuwepo kwenye moja ila penzi halikumwendea vizuri.

“Wanaume wengi wanataka kutoka na mimi sababu wanafikiri nina pesa nyingi. Isitoshe ni vigumu sana kujua nia ya mwanaume anapokutaka mahusiano na wewe upo kwenye tasnia ya muziki. Unakuwa haujui ikiwa anataka tu kupata sifa kuwa anatoka na wewe au kafuata hela kwako,” akasema.

Miezi kadhaa iliyopita msupa huyu alifichua kwamba alijaribu kuwa kwenye mahusiano na msanii mwenzake Arrow Bowy lakini mambo yakagonga mwamba.