Makala

KASHESHE: Sanaipei, Kavutha mbioni kusaka vipaji vibichi

October 11th, 2019 1 min read

Na THOMAS MATIKO

WANAMUZIKI wa siku nyingi Sanapei Tande na Kavutha Mwanzia Asiyo leo wataendelea na usahili wa kusaka vipaji vipya vya uimbaji vitakavyoshindania Sh10 milioni katika shindano jipya la Old Mutual Amazing Voices.

Staa hao ambao wamepewa kazi ya ujaji, wanatakiwa kuibuka na wanamuziki watatu ambao vipaji vyao vya uimbaji havijawahi kusikika.

Baada ya usahili, watatu hao watakaokuwa wamefuzu, watasafiri hadi Afrika Kusini na kujumuika na wengine watakaokuwa wamefuzu kutoka mataifa ya Ghana, Afrika Kusini na Zimbabwe.

Huko ndiko safari ya mchujo itakapoanza kwenye shindano hilo litakalodumu kwa wiki 13. Atakayeibuka mshindi ndiye atakayezawadiwa kitita hicho kizito.

Usahili ulishafanyika mjini Mombasa katikati ya wiki huku leo zoezi hilo likipigwa mjini Nairobi katika afisi za UAP Old Mutual, Upperhill.