Michezo

Kashiwa Reysol ya Olunga sasa yaongoza vita vya kurejea Ligi Kuu ya Japan

August 1st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI Michael Olunga alikuwa uwanjani dakika zote 90 klabu yake ya Kashiwa Reysol ikititiga Okayama 4-0 kwenye Ligi ya Daraja la Pili ya Japan, Julai 31, 2019.

Mabao ya Yusuke Segawa dakika ya pili, Ataru Esaka katika dakika ya saba na Matheus Savio dakika ya 89 pamoja na la kujifunga kutoka kwa Choi Jun-won dakika ya 47 yalitosha kupatia Reysol ushindi wa saba mfululizo inapojikaza kurejea kwenye Ligi Kuu baada ya kutemwa mwaka 2018.

Reysol ya kocha raia wa Brazil, Nelsinho Baptista sasa imechukua uongozi wa ligi hiyo ya klabu 22 kutoka kwa Kyoto Sanga iliyokabwa 1-1 dhidi ya nambari 11 Kanazawa.

Iko juu ya jedwali kwa alama 49 kutokana na mechi 25, alama mbili mbele ya Kyoto Sanga nazo Mito HollyHock, Omiya Ardija na Montedio Yamagata zinafunga mduara wa tano-bora kwa alama 44, 43 na 43, mtawalia. Olunga amefungia Reysol mabao manane na kumega pasi mbili zilizozalisha magoli katika mechi 15 za ligi ameshiriki.

Vijana wa Baptista wataalika nambari 15 Ryukyu katika mechi yao ijayo mnamo Agosti 4 uwanjani Kashiwa Hitachi.

Timu mbili za kwanza baada ya kila mmoja wao kusakata mechi 42, zitaingia Ligi Kuu moja kwa moja. Nambari tatu hadi sita zitapigania tiketi nyingine moja ya kushiriki Ligi Kuu.