Michezo

Kashiwa Reysol ya Olunga yala sare

September 1st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

REKODI ya viongozi Kashiwa Reysol ya kushinda mechi 11 mfululizo kwenye Ligi ya Daraja ya Pili ya Japan imevunjwa na Albirex Niigata baada ya kukabwa 1-1, Jumamosi.

Kashiwa, ambayo imeajiri mshambuliaji Mkenya Michael Olunga, ilikuwa imepiga Gifu (4-0), V-Varen Nagasaki (2-1), Renofa Yamaguchi (4-1), Ryukyu (5-1), Okayama (4-0), Tichigi (2-1), Kanazawa (1-0), Tokushima (2-1), Kofu (4-2), Montedio Yamagata (1-0) na Chiba (2-0) kabla ya kutolewa jasho na Niigata.

Wageni Niigata walitangulia kuona lango kupitia mvamizi wa Mbrazil Leonardo,22, dakika ya 13 uwanjani Hitachi Kashiwa.

Wenyeji walijikakamua na kupata bao la kusawazisha kupitia kwa kiungo Mbrazil Matheus Savio,22, dakika ya 63.

Matokeo haya si mabaya sana kwa Kashiwa inayosalia juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 22 kwa alama 62 kutokana na mechi 30.

Ilinufaika kuwa alama 10 mbele ya wapinzani wake wa karibu nambari mbili Yokohama, nambari tatu Kyoto na nambari nne Omiya Ardija walioteleza. Nambari tano Montedio Yamagata iko alama 11 nyuma ya Kashiwa. Ilipoteza fursa ya kurukia nafasi ya pili baada ya kutoka 0-0 dhidi ya Yokohama. Kashiwa itaalika Montedio Yamagata katika mechi yake ijayo Septemba 7.