Habari Mseto

Kasisi akanusha kughushi hati kumiliki hospitali

May 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KASISI  kutoka Amerika anayezozania umiliki na usimamizi wa hospitali ya kimisheni ya St Marys Lang’ata  alishtakiwa Jumanne kwa ufisadi.

Kasisi William Charles Fryda wa kitengo cha Maryknoll Fathers & Brothers cha Marekani alikanusha mashtaka matatu ya ughushi, kujitengenezea hati na kufanya njama za kutekeleza ufisadi.

Kasisi Fryda alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

Kasisi huyo alishtakiwa kwa kughushi barua ya maafiisa waliokuwa wanaruhusiwa kutia saini katika akaunti ya hospitali hiyo ya St Marys kwenye benki ya  Prime (PB) miaka mitano iliyopita.

Alishtakiwa kutekeleza uhalifu huo mnamo Septemba 17, 2103 mahala pasipojulikana humu nchini.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000.