Siasa

Katiba: Uhuru, Raila kuongoza ukusanyaji sahihi

October 24th, 2020 1 min read

Na DAVID MWERE

CHAMA cha Jubilee ambacho kiongozi wake ni Rais Uhuru Kenyatta na kile cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga vimeteua wanasiasa watakaoongoza shughuli ya kukusanya sahini milioni moja zinazohijatika kubadilisha katiba kupitia kwa jopo la maridhiano la BBI.

Shughuli ya kukusanya sahini hizi inafuatia kuchapishwa kwa Mswada wa kubadilisha Katiba ya Kenya, 2020 katika Gazeti rasmi la Serikali kufuatia kukabidhiwa kwa ripoti ya BBI kwa Rais Kenyatta Jumatano wiki iliyopita katika Ikulu Ndogo ya Kisii.

Wanasiasa hao wataongoza maeneo yao katika kupigia debe mchakato huo na watakuwa wanaripoti kila wiki kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga kuhusu ufanisi wa shughuli hiyo.

Wanasiasa hao watashirikiana na wabunge walio waaminifu kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga kufanikisha mchakato huo unaoungwa mkono na Serikali.

Katika eneo la Pwani, Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Hassan Joho na Gavana wa Kilifi Amason Kingi wataongoza kampeini hizo za kubadilisha katiba kupitia kwa BBI.

Kundi la Joho litawashirikisha Maseneta Mohamed Faki (Mombasa), Stewart Madzayo (Kilifi) na Dkt Agnes Zani (maalum) pamoja na wabunge Dkt Naomi Shaban (Taveta), na Mishi Mboko (Likoni) miongoni mwa wengine.

Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Bw Amos Kimunya aliye pia Mbunge wa Kipipiri na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth wataongoza kundi la eneo la Kati nchini.

“Tuko tayari kuanza mchakato huo lakini tunawahimiza Wakenya wasome ripoti hii ya BBI kwa makini ndipo; wasije wakapotoshwa na wanasiasa walio na ubinafsi na kujipendelea,” alidai Bw Kimunya.

Akaongeza: “Tumeisoma ripoti hii na tutaiunga mkono.”

Kifungu nambari 257 (1) cha Katiba kinasema kwamba kuwa inaweza kufanyiwa marekebisho katika pendekezo lililotiwa sahini na watu milioni moja.