Habari Mseto

Katibu anayehusika na nyumba na makazi aahidi serikali itaboresha Kiandutu

May 21st, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MPANGO wa kazi kwa vijana mitaani utazidi kuboreshwa zaidi ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la Covid-19.

Katibu Mkuu katika Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Mijini Bw Charles Hinga alisema Jumatano serikali ina mpango mwafaka wa kuhakikisha vijana wa hapa nchini wanapata mbinu na shughuli ambazo zinaweza kuwapa ujira.

Alisema ameridhishwa na kazi inayoendelea katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika kwa sababu vijana wameonyesha bidii ya kufanya kazi bila kubagua.

Hivi majuzi serikali iliajiri vijana 1,500 kutoka vijiji vya Kiang’ombe na Kiandutu ili wasaidie kufyeka mitaani na kuzibua mitaro ya majitaka katika mji wa Thika na vitongoji vyake.

Baadhi ya vijana wa kutoka kijiji cha Kiandutu wafyeka Mei 20, 2020, katika mradi wa ‘Kazi kwa Vijana Kupitia Covid-19’. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema serikali imebuni mpango maalum wa kuajiri vijana 26,114 kutoka katika kaunti nane za humu nchini.

Baadhi ya kaunti hizo ni Nairobi, Mombasa, Kilifi, Kwale, Nakuru, na Kiambu.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba kijiji cha Kiandutu kinafanyiwa mabadiliko kutoka miundomsingi hadi nyumba za kisasa.

“Kazi zote zitakazoendeshwa katika kijiji hicho zitafanywa na vijana wa huko na hiyo ni njia mojawapo ya kubuni kazi kwa vijana,” alisema Bw Hinga.

Alisema vijana watakuwa wakilipwa fedha zao kupitia M-Pesa.

Alisema mradi huo wa vijana umegharimu takribani Sh354 milioni na serikali itahakikisha kila kitu kinaendeshwa jinsi inavyostahili.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, aliwashauri wakazi wa Thika wafuate sheria zote za afya ili “tuweze kukabiliana na janga la Covid-19.”

“Tayari hospitali ya Tigoni imegeuzwa kuwa Kiambu Covid-19 Centre Limuru. Nayo Thika Level 5 imetenga chumba chenye vitanda 20 kwa wagonjwa wa Covid-19,”alisema Dkt Nyoro.

Alibainisha kwamba Kaunti ya Kiambu imetenga Sh153 milioni zitakazotumika kwa minajili ya kuunda barabara za kuingia maeneo ya mashinani na umeme kusambazwa katika njia za kupitia mitaani.

Alisema wanapanga kuajiri wafanyakazi wapya ifikapo Julai mosi na hiyo itafanyika tu kwa watu wenye mienendo na tabia njema vijijini.

Kamishna wa Kiambu Bw Wilson Wanyanga alisema kazi kwa vijana inaendelea vyema na tayari maeneo yaliyonufaika na mradi huo ni Kiandutu, Kibarage, Kikuyu, Kiang’ombe, na Kiambu.

“Serikali itaendelea kuona ya kwamba vijana wanapata nafasi ya ajira ili kupunguza uhuni unaoshuhudiwa kila mara. Hata siku hizi uhalifu umepungua kwa kiwango kikubwa katika kaunti nzima ya Kambu,” alisema Bw Wanyanga.

Wakazi wa Kiandutu walipojitokeza kuzungumza walipongeza serikali kwa kazi njema ambayo imefanya ya kuwajali vijana lakini walitaja mambo kadha waliyotaka yarekebishwe.

Walisema wangetaka vyoo vijengwe kwa wingi, huku wakitaka pia njia za kuingia maeneo ya ndani zipanuliwe kwa wingi.