Habari Mseto

Katibu wa zamani apewa fidia ya Sh1 na mahakama

October 23rd, 2020 2 min read

Na SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA moja ya Nairobi inayoshughulikia kesi za Ajira na Kazi imeamuru kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa maswala ya Vijana na Jinsia, Bi Lillian Omollo alipwe Sh1 kama fidia kwa kuachishwa kazi kinyume cha sheria.

Jaji Stephen Radido alisema kwamba, kuachishwa kazi kwa Bi Omollo kulikuwa kinyume na katiba, na akaiagiza serikali imlipe Shilingi moja kwa ukiukaji wa haki zake.

“Mlalamishi hakuchukuliwa hatua zinazostahili, wala hakupewa sababu za kuondolewa ofisini. Baadaye aliarifiwa kuwa muda wake wa kuhudumu umemalizika na mtu mwingine alikuwa ameteuliwa kurithi nafasi yake,” alisema Jaji Radido.

Jaji huyo alisema maafisa wa umma wana matarajio kuwa kulingana na vyeo vyao, utaratibu unaofaa kama inavyotarajiwa chini ya kifungu cha 236 cha Katiba, utazingatiwa wakati wa kuondolewa kwao ofisini.

Hata hivyo, Jaji Radido alisema kwa sababu Bi Omollo, ambaye kwa sasa anapambana na mashtaka ya ufisadi, aligundulika kuwa na utajiri usioelezeka, kiwango alichopewa cha shilingi moja ni fidia ya kutosha kwa kukiukwa haki zake alipoachishwa kazi bila utaratibu kufuatwa.

Bi Omollo tayari amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, ambayo iligundua kuwa zaidi ya Sh33 milioni zilizokuwa katika akaunti zake, hazikuwa halali.

Bi Omollo aliishtaki serikali kupitia kwa Wizara ya Huduma ya Umma na Jinsia akisema kwamba, bado hana hatia na alikuwa na haki ya kulipwa nusu kiwango cha mshahara wake, kwani kesi ya ufisadi inayomkabili inaendelea kortini.

Alikuwa ameteuliwa kama Katibu wa Wizara ya Vijana mnamo Desemba 2015. Na aliposhtakiwa kwa ufisadi kati ya makosa mengine mnamo 2018, aliarifiwa kusimamishwa kazi na kulipwa nusuya mshahara akisubiri kukamilika kwa mashtaka hayo ya jinai.

Aandikiwa barua

Mnamo Mei 2020, Waziri wa Utumishi wa Umma alimwandikia barua kwamba muda wake wa kuhudumu kama katibu ulikuwa umekwisha na mtu mwingine alikuwa tayari ashateuliwa kuchukua nafasi yake.

Uamuzi huo ulimchochea kuenda kortini, akitafuta agizo kutoka kortini kuwa kusimamishwa kazi kwake kulikuwa ni kinyume cha katiba, miongoni mwa maagizo mengine.

Hata hivyo, serikali ilisema kuwa Bi Omollo alishikilia ofisi chini ya uaminifu wa umma, na kwa sababu alikuwa ameshtakiwa kwa makosa ya ufisadi, alisimamishwa kazi kama ilivyotarajiwa chini ya kifungu cha 62 cha Sheria ya Kupambana na Rushwa na Uhalifu wa Kiuchumi.